Wizara ya Maji

Dar es Salaam Water Supply And Sanitation Authority (DAWASA)

TIRA Logo
UBUNIFU NA UZALENDO DAWASA VYAMKOSHA NAIBU WAZIRI WA MAJI
05 Sep, 2023
UBUNIFU NA UZALENDO DAWASA VYAMKOSHA NAIBU WAZIRI WA MAJI

Naibu Waziri wa Maji, Mhe. Mhandisi Maryprisca Mahundi ameipongeza Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) kwa kuwa wabunifu, wazalendo na wenye ari katika usanifu na utekelezaji wa miradi ya Majitaka na uboreshaji wa usafi wa mazingira.

Amesema kuwa miradi hii ambayo ameitembelea ikiwemo ya ujenzi wa vituo vya huduma za usafi wa mazingira kwa jamii na ujenzi wa mfumo wa kukusanya majitaka Mbezi Beach ni miradi ya mfano nchini ambayo imelenga kuboresha Usafi wa Mazingira  na afya za wakazi  Dar es Salaam.

"Nimetembelea utekelezaji wa miradi hii na nimeona ufanisi wa hali ya juu.  Nitoe wito kwa Mamlaka nyingine nchini kujifunza kwa DAWASA namna ya  kubuni na kutekeleza miradi yenye kuakisi hali halisi ya  uboreshaji wa usafi wa mazingira katika maeneo yao," ameeleza Mhandisi Maryprisca.

Mpaka sasa mradi wa ujenzi wa mfumo wa Usafi wa Mazingira Mbezi Beach umeanza kwa kasi na utekelezaji upo ndani ya muda kimkataba.

Aidha Serikali kupitia DAWASA imeshatoa malipo ya awali ya bilioni 7 ili kuhakikisha utekelezaji unakwenda kwa kasi.

"Hii ni moja ya jitihada za Serikali chini ya uongozi wa Mhe. Rais Dkt. Samia za kuwekeza fedha za kuboresha maisha ya Watanzania na tayari Wizara tumeshasaini mkataba mkubwa wa kutekeleza miradi mikubwa ya majitaka na usafi wa mazingira katika mikoa mingine," amesema Mhandisi Maryprisca.

Kwa upande wake Mwakilishi wa Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASA, Mhandisi Shabani Mkwanywe amesema kuwa Mamlaka imejipanga kuhakikisha inatekeleza miradi ya usafi wa mazingira yenye uwezo wa kuendana na ongezeko la kiwango cha maji kinachozalishwa pamoja na ongezeko la idadi ya watu katika mkoa wa Dar es Salaam na Pwani.

 

"DAWASA tunatekeleza miradi ya mkakati ya Usafi wa Mazingira inayohusisha ujenzi wa mitambo ya kisasa ya kuchakata majitaka katika maeneo ya Mbezi Beach, Buguruni pamoja na kukarabati mabwawa ya Kurasini ili kuongeza ufanisi," amesema.

Mhandisi Mkwanywe amesema kuwa kwa sasa tunaongeza nguvu kwenye miradi ya uondoshaji majitaka ambayo ni matokeo ya uboreshaji wa huduma ya Majisafi. Hivyo mradi huu wa Mbezi beach, ni wa mfano na unatekelezwa na Serikali kwa ushirikiano na Benki ya Dunia kwa bilioni 120. Katika awamu ya kwanza, mradi unagharimu bilioni 52, ambapo mpaka sasa bilioni 7 malipo ya awamu ya kwanza yameshalipwa.

"Mradi huu ni wa kisasa ambao utahusisha kazi ya kukusanya majitaka toka majumbani na baada ya kuchakatwa katika mtambo wa kisasa utakaojengwa Mbezi Beach, na pamoja na maji, mtambo utazalisha gesi asilia na mbolea," ameeleza Mhandisi Mkwanywe.