SOGEZENI HUDUMA ZA MAJI KWA WANANCHI KUCHOCHEA USAWA WA KIJINSIA - WAZIRI GWAJIMA
SOGEZENI HUDUMA ZA MAJI KWA WANANCHI KUCHOCHEA USAWA WA KIJINSIA - WAZIRI GWAJIMA
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima (Mb) ametoa wito kwa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es salaam (DAWASA) kuongeza kasi ya usambazaji huduma ya maji kwa Wananchi wengi zaidi ili kuchochea Usawa wa Kijinsia
Waziri Gwajima ameyasema hayo alipotembelea banda la DAWASA katika kilele cha tamasha la kutangaza fursa za Maendeleo na kupinga ukatili wa kijinsia iliyobeba kauli mbiu "Zijue fursa kataa ukatili" lililoandaliwa na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum iliyofanyika Jijini Dar es salaam.
Mhe. Waziri ameishukuru DAWASA kwa kuwa miongoni mwa washiriki katika kongamano hilo amesema mapambano ya ukatili wa jinsia yanakwenda sambamba na upatikanaji wa huduma ya maji ili kuleta usawa na kuchochea ustawi wa Jamii.
"Nimefurahi kuona DAWASA imeshiriki katika kongamano hili na tuendelee kushirikiana kwa pamoja, maji ni uhai na lazima tuwasogezee wananchi huduna ili wasihangaike kutafuta. Ukatili wa kijinsia unafanywa sana kwa makundi ya kina Mama na Watoto, tuongeze kasi ya upatikanaji huduma ili kuboresha maisha na ustawi wa Jamii yetu." alisema Mhe. Waziri Gwajima.
Naye Afisa Mawasiliano wa DAWASA ndugu Joseph Mkonyi amefafanua kuwa Mamlaka imefanikiwa kufikisha huduna ya maji ndani ya eneo lake la kihuduma kwa Mkoa wa Dar es salaam na Pwani kwa asilimia 95 na hivyo kuisaidia Serikali katika kuleta maendeleo chanya na kukuza uchumi wa Taifa.
“Mhe Waziri, Mamlaka imefanikiwa kutekeleza miradi ya maji maeneo mengi ya Mkoa wa Dar es salaam, tunajivunia kukamilisha miradi mbambali inayoboresha maisha ya Wananchi wetu mfano maeneo mapya yaliyopata huduma kama vile Mivumoni, Goba, Madale, Makongo, Mshikamano, Pugu, Ukonga, Chalinze, Mkuranga na maeneo mengine mengi.” Alisisitiza ndugu Mkonyi