SERIKALI YATOA MATUMAINI WAKAZI WA MBEZI, UBUNGO NA MSAKUZI
Naibu Waziri wa Maji Mhandisi Maryprisca Mahundi (Mb) amewataka wananchi hususani wa Kata ya Mbezi, Ubungo na Msakuzi kusini na Kaskazini ambao ni wanufaika wa mradi wa maji Mshikamano kuwa na subira ya kuunganishiwa na huduma kwa kuwa kazi ya ufundi huwa inatekelezwa kwa kuzingatia taratibu zilizowekwa na Mamlaka.
Ameeleza hayo wakati wa ziara yake ya siku ya pili Mkoani Dar es salaam alipotembelea utekelezaji wa mradi wa maji Mshikamano uliotekelezwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) kwa gharama ya Shilingi.
Amesema kuwa mradi huu wa Mshikamano umetekelezwa kwa ufanisi mkubwa na DAWASA na ni mradi ambao utajibu shida ya maji kwa wananchi wengi wa maeneo haya.
"Tumesikia shuhuda nyingi kutoka kwa wananchi kuwa maeneo haya yalikuwa na ukame kwa mrefu, lakini kwa jitihada kubwa za DAWASA maeneo mengi yameanza kupata maji, tunaishukuru DAWASA kwa namna ambavyo wanaiwakilisha vizuri Wizara ya Maji." ameongeza Mhandisi Maryprisca.
"Wito wangu kwa wananchi ambao wameshalipia maunganisho ya maji wawe na subira kwa kuwa kazi za kiufundi zinatekelezwa kwa utaratibu, tayari vifaa vya maunganisho mapya vimeshanunuliwa na wateja mtaanza kuunganishiwa hivi karibuni," Mhandisi Marryprisca Mahundi Naibu Waziri wa Maji.
Tunampongeza sana Mhe. Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa uzalendo wake wa kutoa fedha za mfuko wa Uviko kiasi cha bilioni 2.5 kwenye mradi wa maendeleo ili wananchi wapate maji.
Nae Mwakilishi wa Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASA Ndugu Shaban Mkwanywe amesema anaishukuru Serikali kwa kuwezesha kutekeleza mradi huu na kuukamilisha.
Mradi huu unatuwezesha kujibu hoja za shida ya maji kwa wananchi, kwa sasa kazi tunayoendelea nayo ni kusambaza maji kwa wananchi kwa kasi.
"Kwa mwaka huu wa fedha 2023/24 tumetenga fedha za ndani bilioni 2.5 kwa ajili ya kusambaza maji kwa wananchi wote wa kata ya Mbezi, Msakuzi kusini na kaskazini kuwa wasiwe na wasiwasi huduma itafika," ameeleza Mhandisi Mkwanywe.
Mkazi wa Kata ya Mshikamano Ndugu Sanga Mbowe ameishukuru Serikali kupitia DAWASA na kuomba kazi ya kusambaza maji ifanyike kwa haraka ili wananchi wote waweze kunufaika na huduma.