Wizara ya Maji

Dar es Salaam Water Supply And Sanitation Authority (DAWASA)

TIRA Logo
SERIKALI, DAWASA YAWEKEZA BILIONI 40 KUPELEKA MAJI MAJIMBO MANNE
05 Sep, 2023
SERIKALI, DAWASA YAWEKEZA BILIONI 40 KUPELEKA MAJI MAJIMBO MANNE

Naibu Waziri wa Maji Mhe. Mhandisi Maryprisca Mahundi ametembelea na kukagua maandalizi ya utekelezaji wa mradi wa maji Bangulo unaotarajiwa kunufaisha wakazi wa majimbo manne ya uchaguzi ikiwemo Ukonga, Segerea, Ubungo na Kibamba na huduma ya Majisafi kwa gharama ya zaidi ya bilioni 40.

Amesema kuwa Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuzingatia uhitaji wa maji uliopo kwa wananchi wa majimbo haya hususani wakazi wa Kwembe na Segerea, ameridhia kutoa zaidi ya bilioni 40 za kutekeleza mradi huu mkubwa.

Ameongeza kuwa ujio wa mradi huu ni matokeo ya hoja za wawakilishi wa wananchi wa majimbo haya ya Ukonga, Segerea, Ubungo na Kibamba walizokuwa wakizitoa mara kwa mara bungeni kuhusu changamoto ya maji. Hivyo, Serikali kwa kuzingatia hili imeona umuhimu wa kufika eneo mradi utakapotekelezwa ili kuzungumza na wananchi.

Ameeleza kuwa mradi huu ambao utahusisha ujenzi wa tenki la lita milioni 9 utaondoa kabisa shida ya maji kwenye kata zaidi ya 7. 

"Nipende kuwahakikishia wananchi kuwa Serikali imesikia hoja yenu na jitihada zinafanyika kupitia mradi huu, na sasa Wizara ya Maji kupitia DAWASA inahakikisha Mkandarasi anapatikana na anaanza kazi haraka ili mradi utekelezwe kwa kasi," amesema Mhandisi Maryprisca.

"Nimeridhika na eneo hili la utekelezaji wa mradi huu kwa kuwa kwa hapa huduma itafika kwenye majimbo yote manne, hivyo wananchi wote mjiandae kuoga na kunywa majisafi," amesema Mhandisi Maryprisca.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Miradi DAWASA Mhandisi Ramadhani Mtindasi amesema mradi utahusisha ujenzi wa kituo cha kusukuma maji Kibamba kitakachotumia maji kutoka Ruvu Juu. Pia mradi utalaza bomba kubwa kutoka Kibamba mpaka Bangulo.

Pia mradi utajenga tenki la lita milioni 9 litakalohudumia Wilaya ya Ubungo, Ilala na Kinyerezi. Maeneo ya Kisopwa kwa kulaza bomba kwa umbali wa kilomita 6, Bangulo umbali wa kilomita 12.07, kipinguki kilomita 10.7, maeneo mengine ni kitunda, mzinga, mwanagati yaliyopo jimbo la Ukonga.

Nae Diwani wa Kata ya Pugu Stesheni Mhe. Shabani Musa amesema kuwa mradi huu ni wa mufaa sana kwa wananchi wa majimbo haya hususani Jimbo la Ukonga. 

"Wananchi wengi wakiwemo wa Kwembe na Segerea ambao wamekuwa kwenye shida ya maji kwa muda mrefu wameanza kupata matumaini baada ya kuona nia ya dhati ya Serikali ya awamu ya Sita ya kuwatua ndoo kichwani kupitia mradi huu mkubwa," ameeleza Mhe Musa.

Mradi huu utanufaisha zaidi ya kata zaidi ya 7 za Jimbo la Ukonga na maeneo ya jirani. Hivyo nipende kuwasihi wananchi kuwa watulivu na kuwa tayari kuulinda mradi huu ma miundombinu yote itakayojengwa ili mradi udumu kwa muda mrefu.

Akielezea matumaini aliyonayo kwa mradi huu, mkazi wa Bangulo Bi Ana Sifa ameishukuru Serikali kupitia DAWASA kwa kuona haja ya kuleta mradi huu ili waondokane na changamoto ya maji katika eneo lao.

Amesema kwa sasa maji wanapata kwa shida kutoka na msukumo mdogo unaosababishwa na mwinuko uliopo kwenye eneo hilo. "Niwapongeze sana na niwaombe kutekeleza mradi huu kwa haraka ili tuweze kupata unafuu maana kwa sasa tunanunua maji kwa gharama kubwa," ameeleza