RC CHALAMILA ATETA NA WATENDAJI DAWASA NA TANESCO
Kwa pamoja wamekubaliana kuimarisha huduma kwa wananchi
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe Albert Chalamila amekutana na kufanya kikao kazi na Viongozi waandamizi wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es salaan (DAWASA) na Shirika la Umeme Nchini (TANESCO) kwa lengo la kuzungumza juu ya uimarishaji huduma katika Mkoa wa Dar es salaam.
Akiongea wakati wa kikao hicho Mhe Chalamila amezitaka Taasisi hizo mbili kufanya kazi kwa kushirikiana, pamoja na kuwa na mahusiano ya karibu ya kikazi ili kuwa na matokeo yenye tija yatakayosaidia kutoa huduma bora kwa Jamii wakati wote
Aidha Mhe Chalamila amesema Mkoa wa Dar es Salaam ni mji wa kibiashara, kidiplomasia na kiuchumi, whivyo huduma za Maji na Umeme zinapokosekana huketa athari kubwa ya kuzorotesha mnyororo mzima wa uchumi wa Nchi.
" Natamani kuona Mkoa wa Dar es Salaam hauna changamoto au migao ya aina yoyote iwe ya Maji au Umeme kutokana na umuhimu wa Mkoa huu kuwa kitovu cha uchumi wa Nchi" Alisema Mhe Chalamila
Sambamba na hilo Mhe Chalamila amefafanua kuwa uwepo wa nishati ya umeme husaidia maji huzalishwa kwa wingi na maji yakizalishwa kwa wingi husaidia kwa sehemu kubwa kukabiliana na magonjwa ya milipuko kama vile kipindupindu.