RC CHALAMILA APONGEZA JITIHADA UBORESHAJI USAFI WA MAZINGIRA DAR
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe. Albert Chalamila ameipongeza Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) kwa kuanza utekelezaji wa mradi wa uondoshaji majitaka utakaosaidia kuboresha usafi wa mazingira Dar es Salaam.
Amesema kuwa huu ni mradi wa mfano na mahususi ambao Serikali ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imewekeza fedha nyingi kuonesha nia ya dhati ya Mhe. Rais ya kuboresha afya za wananchi wake na kuwa na makazi salama.
Ameongeza kuwa maendeleo ya nchi yanachochewa na uwepo wa afya bora wa wananchi wake, hivyo mradi huu wa uondoshaji majitaka majumbani ni mwanzo wa mkakati bora wa Serikali wa kuboresha afya ya wananchi wake.
"Hapa Serikali imewekeza fedha dola milioni 65, ambazo zitaboresha usafi wa mazingira kwenye Kata nne ikiwemo Kawe, Kunduchi, Wazo na Mbezi, hivyo huu mradi sio wa mdogo na wananchi wanapaswa kuelewa hivyo,"ameeleza Mhe. Chalamila.
Amebainishwa kuwa huu ni mradi muhimu hasa katika kipindi hiki cha msimu wa mvua za Eli-nino kwa kuwa utatusaidia kuepukana na athari za uchafuzi wa Mazingira ambao huwa unatokea mara kwa mara kwa wananchi kutiririsha majitaka wakati wa mvua.
"Niwatake wananchi wanaopitiwa na mradi huu kutoa ushirikiano kipindi hiki cha utekelezaji ili mradi ukamilike kwa wakati," ameeleza.
Awali akimkaribisha Mkuu wa Mkoa Dar es Salaam, Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Mhe. Sadi Mtambile amesema kuwa mradi huu ni kielelezo kikubwa kwa kuwa asilimia 60 ya magonjwa yanayotokea Dar es Salaam huchangiwa na majimachafu, kupitia mradi huu changamoto ya uchafuzi wa Mazingira itaenda kuisha.
"Huu ni mwanzo wa safari ya kuboresha usafi wa mazingira na tumeanza kwenye kata hizi nne, na kazi itaendelea kuhakikisha Kata zote 20 za Wilaya hii zinanufaika na miradi ya namna hii," ameeleza Mhe. Mtambile.
Kwa upande wake Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASA Ndugu Kiula Kingu hii ni mojawapo ya jitihada za Serikali za kuboresha usafi wa mazingira kwa Dar es Salaam ambapo kupitia mradi huu Kata ya Kawe, Kunduchi, Wazo na Mbezi Juu zitanufaika na uboreshwaji wa usafi wa mazingira.
Mradi huu umesanifiwa kuwa na uwezo wa kuchakata lita milioni 16 kwa saa na kuweza kuzalisha gesi itakayoweza kutumika majumbani, pia utazalisha na mbolea itakayotumika kutunza mazingira yanayouzunguka mtambo.
Amesema kuwa mradi umegharimu dola milioni 65 na utanufaisha wananchi 11488 wa Kata zilizotajwa.
Nae Mwenyekiti wa mtaa wa Mbezi beach Asha George ameeleza kuwa huu mradi unatija kubwa kwenye mtaa wetu mbali na kuboresha usafi wa mazingira, umefungua fursa za ajira kwa vijana wengi.
"Tunaishukuru sana Serikali kwa jitihada hizi za kuboresha usafi wa mazingira kwa kuwa itawaondolea wakazi wa huku na shida ya uchafuzi wa Mazingira," ameeleza Mhe Chalamila.