Wizara ya Maji

Dar es Salaam Water Supply And Sanitation Authority (DAWASA)

TIRA Logo
PROF KITILA AIPA TANO DAWASA USIMAMIZI WA MIRADI YA USAFI WA MAZINGIRA
29 Sep, 2023
PROF KITILA AIPA TANO DAWASA USIMAMIZI WA MIRADI YA USAFI WA MAZINGIRA

Kaya zaidi ya 200 Sinza - Kijitonyama kuwa kitovu cha usafi wa mazingira Dar

Mbunge wa Jimbo la Ubungo Mhe. Prof. Kitila Mkumbo ameipongeza Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) kwa utekelezaji wa mradi wa uondoshaji majitaka na kuwataka kuweka mkakati na bajeti maalum kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya Majitaka.

Ameyasema hayo wakati wa ziara ya kutembelea na kukagua maendeleo ya mradi wa uondoshaji majitaka wa PSSSF unaotekelezwa na Mamlaka kwenye maeneo ya Sinza - Kijitonyama kwa lengo la kumaliza changamoto ya uchafuzi wa Mazingira katika maeneo hayo.

Amesema kuwa anaipongeza DAWASA kwa kutekeleza mradi wa PSSSF kwa ufanisi na kuwataka kuongeza nguvu kwa kuweka bajeti ya kutekeleza miradi hii ili kuondoa adha ya uchafuzi wa Mazingira katika Kata ya Sinza.

"Changamoto kubwa iliyopo sasa kwenye maeneo ya Sinza ni uchafuzi wa Mazingira unaosababishwa na utiririshaji hovyo wa majitaka kwenye makazi ya watu, lakini kupitia mradi huu, adha hii itaisha kabisa na utaleta faraja kwa wakazi wengi," ameeleza Prof. Mkumbo.

Ameongeza kuwa, kwa sasa DAWASA ni wakati muafaka wa kuweka mkakati madhubuti wa kutekeleza miradi ya Majitaka ili kuokoa uchafuzi wa Mazingira kwenye maeneo mengi hususani Kata ya Sinza, Manzese, Kijitonyama nk.

"Hivyo niwajulishe wakazi wa Sinza kwamba ahadi ya Serikali ya Mhe. Rais Dkt Samia Suluhu Hassan ya kuondoa adha ya uchafuzi wa Mazingira imesikiwa na kazi mdo hii inaendelea, hivyo niwatake wananchi watakaonufaika kuacha kutupa taka hovyo kwenye miundombinu hii kwa kuwa Serikali imewekeza fedha nyingi kwenye mradi huu," ameeleza Mhe. Mkumbo.

Kwa upande wake Meneja wa Miradi PSSSF Mhandisi Marko Kapinga ambao ni wanufaika wa mradi amesema kuwa mradi huu una manufaa makubwa kuanzia kwa wapangaji wa jengo letu la PSSSF pamoja na wakazi wanaozunguka jengo hili na utapunguza kwa kiasi kikubwa magonjwa ya mlipuko yanayosababishwa na utiririshaji hovyo wa majitaka mitaani.

"Hivyo ni jukumu la kila mmoja wetu kuhakikisha mradi huu unalindwa kwa kuwa umetumia fedha nyingi za Serikali, ili mradi udumu na kunufaisha wakazi wote," ameeleza Mhandisi Kapinga.

Mwakilishi wa Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASA Mhandisi Modesta Mushi ameeleza kuwa utekelezaji wa mradi unalenga kunufaisha kaya zaidi ya 200 za mitaa ya Sinza A, B, C pamoja na hospitali ya Palestina, kwa kuziondolea changamoto ya uchafuzi wa Mazingira na kuboresha usafi wa mazingira.

"Mradi ulianza kutekelezwa mwezi Mei mwaka huu, ambapo tunalaza bomba la inchi 12 kwa umbali wa kilomita 2.886. Mpaka sasa, tumelaza bomba kwa umbali wa kilomita 1.344 sawa na asilimia 47 ya utekelezaji," ameeleza Mhandisi Modesta.

"Tumejipanga kikamilifu kukamilisha mradi huu mwezi wa kumi, kwa kuwa inatekelezwa usiku na mchana, niwasihi wananchi kuacha kutupa taka ngumu kwenye miundombinu hii kwa kuwa inasababisha kuziba na kuchelewesha ukamilishwaji wa mradi," amesema Mhandisi Modesta.

Ameishukuru PSSSF kwa kutoa ushirikiano wa utekelezaji wa mradi huu unaoleta manufaa ya afya kwa pande zote. 

Ameahidi kuwa DAWASA itaendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu namna bora ya kuondosha majitaka bila kuchafua Mazingira na bila kuharibu miundombinu, amesihi wananchi kufika katika ofisi za Mamlaka kwa taarifa zaidi.