NAIBU WAZIRI MAJI ATEMBELEA MRADI WA BWAWA LA KIDUNDA
Naibu Waziri wa Maji Mhe. Mhandisi Maryprisca Mahundi (Mb) ameridhishwa na kasi ya utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa Bwawa la kuhifadhi maji la Kidunda chini ya usimamizi wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es salaam (DAWASA) huku akibainisha mradi huo utakavyosaidia kupunguza changamoto ya upungufu wa maji katika mikoa ya Pwani na Dar es salaam wakati wa kiangazi.
Mhandisi Mahundi ameibanisha hayo wakati wa muendelezo wa ziara yake katika miradi inayosimamiwa na DAWASA ambapo mradi wa kidunda unatekelezwa katika Kata ya Mkulazi Mkoani Morogoro.
"Tunamshukuru Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuridhia kiasi cha fedha zaidi ya bilioni 300 kwa ajili ya mradi huu wenye manufaa makubwa sio tu kwa wakazi wa mikoa ya Dar es salaam na Pwani bali kwa wananchi wa eneo hili. Nimeshuhudia kupitia mradi huu barabara ya umbali wa kilomita 75 imeboreshwa, wananchi wazawa wamepata ajira za muda mfupi, ujenzi wa huduma za kijamii ikiwemo shule na zahanati zimejengwa." amesema Mhandisi Mahundi
Pia ametoa wito kwa DAWASA kuendeleza ushirikiano na wakazi wa Kijiji cha Kidunda ili kurahisisha mazingira ya kazi kwa mkandarasi na amewataka wakazi hao kuwa mstari wa mbele wa kulinda miundombinu ya maji, na kujiepusha na vitendo vya ubadhilifu wa mali za mradi ili uweze kukamilika kwa wakati.
Kwa upande wake Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es salaam (DAWASA) Ndugu Kiula Kingu amesema kuwa mradi wa Kidunda unategemewa kuwa mwarobaini wa upungufu wa maji wakati wa kiangazi ambapo unatarajiwa kuhifadhi maji kiasi cha lita milioni 190 kwa mwaka na kuwezesha mitambo ya kuzalisha maji ya Ruvu Juu na Ruvu Chini kuzalisha maji kwa mwaka mzima bila changamoto yeyote.
"Tunaishukuru Serikali ya awamu ya sita kwa kuidhinisha fedha za awali takribani bilioni 49 zilizomsaidia mkandarasi kuanza mwezi wa sita mwaka huu na ambapo tunategemea utekelezaji utafanyika kwa kasi, tuna uhakika mradi utakamilika kwa wakati uliowekwa kimkataba." amesema Ndugu Kingu
Alizungumza kwa niaba ya wananchi wa Kidunda Mwenyekiti wa Kijiji cha Kidunda Ndugu Ramadhani Mwite ameshukuru Serikali ya awamu ya sita kwa kuwaletea mradi huu mkubwa ambao utaenda kuleta maendeleo katika kijiji cha Kidunda pia amewapongeza DAWASA kwa ushirikiano mzuri waliouonesha tangia mwanzo wa mradi hadi kufikia hatua hii ya utekelezaji.
Aidha ziara hii ilihudhuriwa na wawakilishi kutoka ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Mkuu wa Wilaya ya Morogoro na Mkurugenzi wa Mamlaka ya Bonde la Wami Ruvu.