Wizara ya Maji

Dar es Salaam Water Supply And Sanitation Authority (DAWASA)

TIRA Logo
NAIBU WAZIRI MAJI AITAKA DAWASA KUUNGANISHA MAJI KWA MKOPO MRADI WA CHALINZE
06 Sep, 2023
NAIBU WAZIRI MAJI AITAKA DAWASA KUUNGANISHA MAJI KWA MKOPO MRADI WA CHALINZE

Naibu Waziri wa Maji Mhe. Mhandisi Maryprisca Mahundi (Mb) ameitaka Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es salaam (DAWASA) kuwaunganisha  wanufaika wa Mradi wa maji wa Chalinze awamu ya tatu na huduma ya majisafi kwa mkopo baada ya kukamilika kwa mradi huo.

Amesema hayo wakati akizungumza na wanachi wa kijiji cha Kihangaiko, Kata ya Msata, Halmashauri ya Chalinze Wilaya ya Bagamoyo kwenye mkutano wa hadhara baada ya ziara ya kukagua upanuzi wa Mtambo wa kuzalisha maji wa Wami ambayo ni moja ya shughuli zilizofanyika kwenye utekelezaji wa mradi huu.

"Kwanza kabisa namshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu kwa kuendeleza jitihada za kuhakikisha adhma ya kumtua mama ndoo kichwani inafanyika kwa vitendo, pia niwapongeze watendaji wa DAWASA hakika kazi ya utekelezaji wa mradi huu ni nzuri na inaonekana" amesema Mhandisi Mahundi

Aidha, Mhandisi Mahundi ametoa maagizo kwa DAWASA ya kuwaunganisha wanufaika wa mradi huo kwa mkopo kwa kuzingatia masharti nafuu na vigezo rafiki ili kila mwananchi apate huduma ya majisafi karibu na makazi yake.

Naye, Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo Mhe. Halima Okashi wakati akimkaribisha Naibu Waziri wa Maji ameipongeza Wizara ya Maji kwa kusimamia vyema utekelezaji wa miradi ya maji katika Wilaya ya Bagamoyo hususani mradi wa maji wa Chalinze awamu ya tatu ambao umeenda kuondoa changamoto ya upatikanaji wa maji iliyokuwepo kwa mda mrefu.

"Tutakuwa wachoyo wa fadhila kama tutaacha kumshukuru Rais wetu msikivu ambaye kwa namna kubwa ametusaidia wanawake wa Wilaya ya Bagamoyo sasa upatikanaji ni wa uhakika, pia tunawapongeza DAWASA kwa kuendelea kuipa ushirikiano ofisi yangu ambao tumezunguka nao kwenye kata zote 26 kusikiliza na kutatua changamoto za wananchi wa wilaya ya Bagamoyo" amesema Mhe. Okashi

Kwa niaba ya Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu Mhandisi Shabani Mkwanywe amesema mradi wa maji wa Chalinze ni moja ya miradi ya mfano ya vijijini kutokana na usanifu mzuri uliofanyika na utaenda kunufaisha takribani vijiji 59 vya Pwani, Morogoro vijijini na Wilaya ya Handeni Tanga.

"Mradi wa maji wa Chalinze awamu ya tatu umehusisha upanuzi wa mtambo wa kuzalisha maji Wami, ulazaji wa bomba za inchi 12 na 16 kwa umbali wa kilomita 24, ujenzi wa matenki ya kuhifadhi maji ya chini na juu takribani 19 na ujenzi wa vizimba vya kuchotea maji takribani 351 na umegharimu zaidi ya bilioni 44 na unategemea kunufaisha wakazi zaidi ya 200,000" ameeleza Mhandisi Mkwanywe

Naye, Diwani wa Kata ya Msata Ndugu Celestin Mcholo amesema anashukuru kwa Serikali kupitia DAWASA kuwaletea mradi mkubwa wa maji ambao umeleta mabadiliko makubwa pia amemshukuru Naibu Waziri kwa kupokea kilio chao cha kufanyiwa maunganisho ya maji kwa mkopo   pia amewaomba wananchi wa Kata ya Msata kutunza miundombinu na vyanzo vya maji   ili kuendelea kupata huduma ya majisafi bili changamoto yeyote.