Mradi wa usafi wa Mazingira wapokelewa kwa hisia tofauti na Wakazi Kawe
Wananchi wa Kata ya Kawe katika mitaa ya Mbezi beach A na Mbezi beach B wamepongeza utekelezaji wa mradi wa Usafi wa Mazingira katika mitaa yao itakayosaidia kuboresha afya na Usafi wa Mazingira unaotekelezwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es salaam (DAWASA)
Wakizungumza wakati wa mkutano na elimu kwa umma ulioandaliwa na DAWASA, mwakilishi wa wananchi ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Kawe Mhe.Dkt.Josephat Gwajima amemshukuru Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuruhusu mradi mkubwa na wa kisasa kuanza kutekelezwa katika jimbo lake.
"Ni faraja kubwa kuona wana Kawe tumekumbukwa na mradi huu mkubwa na wa kihistoria, leo wenzetu DAWASA wamekuja kuutambulisha mradi huu ni kuwaomba wananchi ushirikiano pindi watekelezaji wa mradi watakapotembelea majumbani kwetu, tusiwe kikwazo cha kuchelewesha mradi kukamilika kwa wakati." ameeleza Mhe. Gwajima.
Mheshimiwa Gwajima ameongeza kuwa mradi huu wa unafaida lukuki kwa ikiwemo wananchi waishio katika eneo la mradi kupata kipaumbele cha ajira wakati wa utekelezaji wa mradi na pia kupunguza gharama za kila mwezi za kukodisha magari ya kunyonya majitaka.
Akitoa taarifa ya mradi, msimamizi wa mradi kutoka DAWASA Mhandisi Benard Chonjo ameeleza kuwa mradi utakapokamilika utahudumia zaidi ya kaya 11,400 na hadi sasa kaya 4000 zimeshafanyiwa upimaji wa awali kwaajili ya maunganisho.
"Mpaka sasa jumla ya Kilomita 13 za bomba zimekwisha tandazwa kati ya Kilomita 101, tunawasihi sana wananchi kutoa ushirikiano wa kutosha pindi wataalamu wanaotekeleza mradi wakipita katika makazi yetu Ili kazi hii ikamilike kwa wakati na bila changamoto." ameeleza Mhandisi Chonjo.
Ndugu Mariam Hamduni mkazi wa mtaa Mbezi beach A ameishukuru DAWASA kwa utekelezaji wa mradi ambao ulisubiriwa kwa muda mrefu ili kuboresha Usafi wa Mazingira katika mtaa wao.
"Sasa tunaweza kusema utiririshaji wa majitaka sasa basi, mradi huu utakua na faida kubwa kwetu na tumeupokea kwa moyo mmoja lakini pia tunaridhishwa na Kasi tunayoiona wanaenda nayo mtaani" ameeleza ndugu Mariam.
Faida mbalimbali kupitia mradi huu ambao utatekelezwa kwa kipindi cha Miezi 18 kuanzia Mei 2023 hadi Disemba 2024 ni pamoja na uzalishaji wa umeme utakaotumika kuendesha mtambo, uzalishaji wa gesi, pamoja na upatikanaji wa ajira kipindi cha utekelezaji wa mradi.