MRADI WA USAFI WA MAZINGIRA MBEZI BEACH WATAMBULISHWA RASMI KWA WANANCHI.
Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) imeutambulisha rasmi mradi wa kuchakata majitaka wa Mbezi Beach kwa wakazi wa Kata ya Kunduchi ambao ni sehemu ya wanufaika wa mradi huo.
Akizungumzia utekelezaji wa mradi wakati wa mkutano wa utoaji elimu kwa umma, Mbunge wa Jimbo la Kawe Mhe. Dkt. Josephat Gwajima amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwakuleta mradi huu mkubwa na wa mfano eneo la Mbezi beach.
"Mradi huu ni mzuri na wa mfano kabisa, na ambao utaacha alama ya Usafi wa Mazingira katika Kata yetu ya Kunduchi, naomba sasa wananchi tuupokee kwa moyo mmoja na kutoa ushirikiano wa kutosha kwa wanatumishi wanaotekeleza huu mradi pindi wanapotembelea majumbani mwetu kutekeleza majukumu yao," ameeleza Mhe. Gwajima.
Mhe. Gwajima ameongeza kwa kuwatoa wasiwasi wakazi wote hasa wa mtaa wa Kilongawima watakaokuwa wanapakana na Mtambo wa kuchakata Majitaka utakaojengwa eneo hilo, kuwa mradi ni salama na hautakua na athari za kimazingira kwao.
"Niwatoe hofu wananchi, mradi huu ni salama kabisa na mtambo huu wa uchakataji majitaka utakua umefunikwa vyema hivyo hautaleta uchafuzi wa Mazingira kama harufu," ameeleza Mhe. Gwajima.
Kwa upande wake Msimamizi wa mradi kutoka DAWASA Mhandisi Benard Chonjo ameeleza kuwa mradi huu unahusisha ujenzi wa mtambo wa kuchakata Majitaka pamoja na uchimbaji na ulazaji wa mtandao wa mabomba kwa umbali wa km 101.
"Kazi imekwisha anza na hadi sasa mtandao wa bomba wa km 12 umeshalazwa, pia hii ni fursa kwa wakazi wa eneo mradi unapotekelezwa kupata ajira kwa kuwa watapewa kipaumbele, hivyo tunawaomba sana wananchi kushirikiana na DAWASA kipindi tutakapotembelea makazi yenu ili kazi iende kwa haraka na usahihi mkubwa," ameeleza Mhandisi Chonjo.
Ndugu Michael Kisanga Mkazi wa mtaa wa Kilongawima ameishukuru Serikali kupitia DAWASA kwakuleta mradi mkubwa katika Kata yao kwani ni jambo walilongoja muda mrefu.
"Sasa Mazingira yetu yatabaki salama na safi, utiririshaji hovyo wa majitaka unaenda kuisha kabisa, mradi huu tuliungoja na tupo tayari kutoa ushirikiano kipindi chote cha utekelezaji wake," ameeleza Ndugu Kisanga.
Pamoja na hayo wananchi wa Kata ya Kunduchi walikumbushwa uwepo wa dawati maalumu la kushughulikia malalamiko kipindi cha utekelezaji wa mradi na kukumbushwa kufika katika ofisi za Serikali ya Mtaa kwa yeyote mwenye changamoto.
Mradi wa Usafi wa Mazingira Mbezi beach unagharimu kiasi cha Dola milioni 65 na utahudumia zaidi ya kaya 11,400 katika Kata ya Kawe, Kunduchi na Wazo ambapo utatekelezwa kwa kipindi cha miezi 18 kuanzia mwezi Mei, 2023 hadi Disemba 2024.