Wizara ya Maji

Dar es Salaam Water Supply And Sanitation Authority (DAWASA)

TIRA Logo
MRADI USAFI WA MAZINGIRA PSSSF SINZA-KIJITONYAMA WASHIKA KASI
05 Sep, 2023
MRADI USAFI WA MAZINGIRA PSSSF SINZA-KIJITONYAMA WASHIKA KASI

Na Fredy Mshiu

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es salaam DAWASA imeendelea kuboresha Usafi wa Mazingira katika eneo lake la kihuduma Ili kuhakikisha Mazingira ya wateja inayowahudumia yanabaki kuwa safi na salama.

Haya yameonekana kupitia utekelezaji wa mradi wa Usafi wa Mazingira PSSSF Sinza-Kijitonyama wenye lengo la kumaliza kabisa changamoto ya uchafuzi wa Mazingira katika eneo hilo.

Akizungumzia utekelezaji wa mradi huo, msimamizi wa mradi, Mhandisi Justine Kyando ameeleza kuwa kazi inakwenda kwa Kasi nzuri na wananchi wategemee huduma Bora kabisa pindi mradi utapokamilika.

"Eneo hili lilikua halina kabisa mtandao wa uondoshaji maji taka, utekelezaji wa mradi huu utamaliza changamoto ya uchafuzi wa Mazingira katika eneo hili na kila mwananchi atanufaika na mradi" ameeleza Mhandisi Kyando

Kyando ameeleza kuwa mradi umehusisha uchimbaji na ulazaji wa bomba za ukubwa wa inchi 12 kwa umbali wa Kilomita 2.8 na mpaka kukamilika kwake takribani chemba 60 za kukusanya majitaka zitajengwa.

Ndugu Maulid Hamduni mkazi wa Kijitonyama ameeleza furaha ya wakazi wa eneo hilo kwa kuona utekelezaji wa mradi huo unaendelea.

"Tunafuraha sana, mtaani tunaona kazi zinazoendelea na zinatutia moyo sana kua Mazingira yetu sasa yatakua safi na salama, tuliitamani huduma hii kwani ni nafuu kwetu na itapunguza gharama za maisha" ameeleza ndugu Maulid

Mradi wa Usafi wa Mazingira PSSSF Sinza-Kijitonyama unaotegemea kukamilika mwishoni mwa mwezi Oktoba 2023, unagharimu kiasi cha shilingi bilioni 1.4 utanufaisha zaidi ya wateja 200 katika maeneo ya Sinza B, Sinza C, Mabatini, pamoja na eneo la Kijitonyama.