MKANDARASI MRADI WA MAJI KWALA AKABIDHIWA SITE RASMI
Mradi wa maji Kwala ni mojawapo ya mradi wa kimkakati ambao umetambulishwa rasmi katika ngazi ya Kata ya Halmashauri ya Kijiji cha Kwala iliyopo Kata ya Kwala, Mkoani Pwani kwa lengo kujenga uelewa na kujenga mahusiano wakati wa utekelezaji wa mradi unaolenga kuboresha upatikanaji wa huduma ya maji kwa wakazi wa Pwani.
Akizungumza wakati wa kutambulisha mradi huo, Mhandisi Bakari Mgaya amesema kuwa mradi huo utachochea ukuaji wa uchumi na kuboresha ustawi wa jamii kwa wakazi wa maeneo hayo mara baada ya kukamilika kwake.
"DAWASA imejipanga kufikisha maji Kwala kwa lengo la kusogeza huduma kwa wananchi, lakini pia kuunga mkono jitihada za Serikali ambayo ilitenga eneo la Kwala kwa ajili ya kuwa Mji wa biashara," ameeleza Mhandisi Mgaya.
Akieleza kazi zinazokwenda kufanyika, Mhandisi Mgaya amesema kuwa mradi unahusisha ujenzi wa matanki sita ya juu yenye uwezo wa kuhifadhi maji zaidi ya lita milioni moja kwa siku, ulazaji wa bomba kuu la chuma la kusafirisha maji la inchi 16 pamoja na ulazaji wa mtandao wa kusafirisha maji kwa kilomita 46 , ulazaji wa bomba la inchi 12 kwa umbali wa kilomita 25.1 na ulazaji wa bomba za inchi 8 na 4 kwa umbali wa Kilomita 46.4
"Kukamilika kwa kazi hizi kutakwenda kuboresha huduma ya maji na kuchangia kuongeza upatikanaji wa huduma ya maji kwa asilimia 95 kwa maeneo ya mjini na 85 kwa vijijini," ameeleza.
Diwani wa Kata ya ya Kwala, Ndugu Mansour Kisebengo amesema amefurahishwa sana na ujio wa mradi huo na kusema mradi utakwenda kuinua wakazi wa Kwala kiuchumi na hata kwa taifa zima.
"Niwashukuru sana DAWASA kwa kutuletea mradi huu hapa kwetu na sio sehemu nyingine kwani utakwenda kututoa kimasomaso katika uchumi," amesema Ndugu Kisebengo.
Mradi wa maji Kwala unatekelezwa na mkandarasi kutoka China Communication Construction Company (CCCC), kwa zaidi ya bilioni 23 ukilenga kunufaisha zaidi ya wakazi 7,900 eneo ya Mji wa Kwala na vitongoji vyake, Bandari kavu.