Wizara ya Maji

Dar es Salaam Water Supply And Sanitation Authority (DAWASA)

TIRA Logo
MIRADI LUKUKI YA MAJI KUTEKELEZWA MAJIMBO YA UCHAGUZI DAR ES SALAAM
06 Sep, 2023
MIRADI LUKUKI YA MAJI KUTEKELEZWA MAJIMBO YA UCHAGUZI DAR ES SALAAM

Serikali kupitia Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) imeanza utekelezaji wa mradi wa maji utakaonufaisha Jimbo la Uchaguzi la Temeke katika kata ya Buza, Vituka, Makangarawe na Sandali pamoja na majimbo mengine matano ya Uchaguzi ya Kibamba, Ubungo, Kinyerezi, Ukonga na Ilala. 

Hayo yameelezwa na Naibu Waziri wa Maji Mhe. Mhandisi Maryprisca Mahundi alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Temeke, Dorothy Kivale aliyehoji ni lini Serikali itapeleka huduma ya maji katika Kata za Buza, Vituka, Makangarawe na Sandali zilizopo Manispaa ya Temeke. 

Amesema kuwa katika kuhakikisha wananchi wa Kata za Buza, Vituka, Makangarawe na Sandali Manispaa ya Temeke wanapata huduma ya maji, Serikali inaendelea na utekelezaji wa mradi wa usambazaji maji wa Jet - Buza ambao hadi kufikia mwezi Agosti 2023, utekelezaji umefikia asilimia 30 na unatarajiwa kukamilika mwezi Juni, 2024. 

Amesema mradi huo utakapokamilika utanufaisha wananchi zaidi ya 173,810 wa Kata hizo. 

"Katika kuboresha huduma ya majisafi kwenye Mkoa wa Dar es Salaam, Serikali katika mwaka wa fedha 2023/24 itaanza utekelezaji wa mradi mkubwa wa maji utakaonufaisha Jimbo la Uchaguzi la Temeke (Kata za Buza, Vituka, Makangarawe na Sandali) pamoja majimbo mengine matano ya Uchaguzi ya Kibamba, Ubungo, Kinyerezi, Ukonga na Ilala. 

"Kaz zilizopangwa kufanyika ni pamoja na ujenzi wa tanki la lita milioni 9 eneo la Bangulo na ulazaji wa mtandao wa mabomba wa umbali wa kilomita 124. Mradi huo unatarajiwa kukamilika ifikapo Desemba 2024," amesema Mhe. Maryprisca