MIKAKATI KUDHIBITI UPOTEVU WA MAJI KWA TEKNOLOJIA YAAINISHWA
Mamlaka ya Majisa na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) imeainisha mkakati kabambe wa miaka mitatu wa kukabiliana na upotevu wa majisafi kwenye eneo lake la kihuduma kwa asilimia 80 kufikia mwaka 2026.
Mojawapo ya mkakati ulioainishwa ni pamoja na kazi ya utambuzi wa mifumo ya kusambaza Majisafi yaliyopo kwenye eneo la kihuduma kwa lengo la kuyaingiza katika mifumo ya taarifa za Kijiografia.
Akizungumzia mkakati huu, Msimamizi wa Kitengo cha Udhibiti wa maji yanayopotea Ndugu Suzan Marko amesema kuwa mpango huu unalenga kuokoa upotevu wa maji yanayopotea kwa kiasi kikubwa ili kuweza kuimarisha upatikanaji wa huduma kwa wananchi.
"Utekelezaji wa mradi huu wa utambuzi wa mifumo umeanza rasmi mwezi Julai ambapo tumepanga kuanzia kwenye mkoa wa kihuduma DAWASA Tabata, na tutaendelea kwenye maeneo mengine ya kihuduma," ameeleza Ndugu Suzan.
Mkakati mwingine ni kufunga mita za kufuatilia kiasi cha maji (bulk meter) katika maeneo yote ya kihuduma ili kutambua kiasi cha maji yanayoingia na yanayotumika kwenye eneo husika.
"Kupitia bulk meters tutaweza kujua kiasi cha maji kinachozalishwa na kinachoelekezwa kwenye matumizi ili kubaini maji yaliyotumika na yaliyopotea," amefafanua Ndugu Suzan.
Mradi huu ni sehemu ya jitihada za Mamlaka za kuokoa upotevu wa maji, na kwa sasa kazi ya kuyatambua mabomba inaendelea ili tuweze kuyafuatilia kupitia mifumo ya teknolojia.
"Katika mradi huu tunafanya kazi ya kuyatambua mabomba yote kuanzia yale makubwa yanayosafirisha maji ya ukubwa wa inchi 72, 54 na 32, pia yale yanayosambaza maji kwenda kwa wananchi kuanzia inchi 16 hadi inchi 1.5," amesema ndugu Suzan.
Mbali na hapo, mradi huu utasaidia kubaini vitendo vya wizi wa maji vinavyofanyika katika mifumo ya maji na kudhibiti ili kuokoa upotevu wa maji na kuboresha huduma.
"Tunaamini kupitia jitihada hizi na kwa kutumia mifumo ya teknolojia itatuwezesha kuweza kukabiliana na upotevu mkubwa wa maji mitaani," amesema ndugu Suzan