MBAGALA WAIPA TANO DAWASA HUPATIKANAJI HUDUMA
Wakazi wa kata za Kijichi na Mbagala Kuu wameipongeza Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) kuimarisha upatikanaji wa uhakika wa huduma ya majisafi katika kata hizo na kutoa nafasi ya kukua kwa uchumi wa Jamii.
Hayo yamesemwa na wakazi mbalimbali waishio katika kata hizo walioonyesha furaha yao ya upatikanaji wa huduma huku wakiipongeza Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mh Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan iliyokusudia kumtua mama ndoo kichwani.
Bi. Magret Mwita mkazi wa Mtoni Kijichi amesema kuwa hapo awali huduma ya maji ilikuwa ikipatikana kupitia visima binafsi na visima vya jumuia hali iliyopelekea watoto wa kike kushindwa kuhudhuria masomo yao kutokana na kutumia muda mrefu kutafuta maji.
"Kiukweli huduma ya maji ya DAWASA imekuwa bora zaidi ukilinganisha na zamani tulivyokuwa tunapata maji kwa tabu hata kupelekea watoto wetu kuchelewa katika masomo yao, ila DAWASA kupitia Serikali imetusaidia sana kutuboreshea huduma". amesema nduguMagret
Nae Amina Juma, mkazi wa Mbagala Misheni mtaa wa Kwa Buruda ameishukuru Serikali kwa kuhakikisha upatikanaji wa maji umekuwa wa uhakika akisem hapo awali ilikuwa ikipatikana kwa umbali mrefu huku gharama zikiwa kubwa kwa ndoo moja.
"Tumekuwa tukitafuta na kufuata huduma ya maji kwa umbali mrefu sana kitu ambacho kilikuwa kinaleta madhara kwenye familia zetu, hata gharama zake zilikuwa kubwa unakuta ndoo kubwa ikiuzwa kwa shilingi 200 na ndogo shilingi 100 ila tangu tupate huduma kupitia DAWASA tunaona unafuu wa huduma ya maji tofauti na visima vya watu binafsi ambao walikuwa wakituuzia kwa gharama kubwa”. amesema ndugu Amina
Mbali na hayo uongozi wa Serikali ya mtaa wa Mbagala Kuu Magharibi kupitia Mwenyekiti wa Shina Ndugu Habibu Msuya amesema kuwa kabla ya mradi wa maji Mgembaki kukabidhiwa kwa DAWASA huduma ya maji haikuwa nzuri kwenye mtaa wake kutokana na changamoto za uendeshaji.
Afisa Huduma kwa wateja DAWASA , ndugu Safina Mukhi ametoa wito na kuwasihi wateja kufanya malipo ya huduma za maji kwa wakati ili kuiwezesha mamlaka kuendelea kutekeleza majukumu yake ya kuwafikishia huduma katika maeneo mengi zaidi.