MAPINDUZI YA TEKNOLOJIA KUBORESHA HUDUMA
Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es salaam (DAWASA) imeimarisha uwekezaji kwenye matumizi ya teknolojia katika utoaji wa huduma kwa wateja ili kuboresha mahusiano mazuri na ukaribu kwa wateja.
Kaimu Mkuu wa Kitengo Cha Tehama DAWASA Ndugu Charles Kayuza amebainisha hayo wakati wa mahojiano maalumu ya kipindi cha radio cha... kuelezea umuhimu wa teknolojia katika utoaji wa huduma za majisafi.
"Ni miaka mitano sasa tangu Mamlaka kuanzisha mifumo mbalimbali iliyosaidia kuboresha utoaji wa huduma ya majisafi kwa wateja ambayo imechochea mafanikio katika taasisi," ameeleza Ndugu Kayuza.
Ndugu Kayuza ameongeza kuwa uwepo wa mifumo hii ikiwemo DAWASA App, umerahisisha mawasiliano baina ya Taasisi na wateja kwani kupitia mifumo hii mteja anaweza kujihudumia kwa kuona matumizi yake ya mwezi ya maji na zaidi kutoa taarifa ya uwepo wa upotevu wa maji kwenye maeneo yao.
"Mteja sasa anaweza kupata ujumbe wake mwenyewe wa ankara ya maji badala ya kusubiri bili za makaratasi, hii imeboresha utoaji wa huduma kuwa wa haraka na kuongeza mapato kwa Mamlaka.
Ndugu Kayuza ameeleza kuwa utumiaji wa teknolojia unasaidia Taasisi kuainisha maeneo yenye uhitaji mkubwa wa maji na kuyapelekea huduma kwa wakati, lakini pia kutambua kiasi cha maji yanayozalishwa na yanayomfikia mteja hivyo kujua kiasi cha maji yanayopotea.
Mamlaka imeendelea kuwekeza katika matumizi ya teknolojia (TEHAMA) ili kuwafikia wateja kwa urahisi na kuwapatia huduma inayofikia na kuvuka matarajio yao, ambapo mpaka sasa jumla ya mifumo miwili mikubwa (DAWASA App, Maji's) inatoa huduma kwa wateja.