Wizara ya Maji

Dar es Salaam Water Supply And Sanitation Authority (DAWASA)

TIRA Logo
MAKAMU WA RAIS ARIDHISHWA UTEKELEZAJI MRADI WA MAJI SAME - MWANGA - KOROGWE
18 Apr, 2024
MAKAMU WA RAIS ARIDHISHWA UTEKELEZAJI MRADI WA MAJI SAME - MWANGA - KOROGWE

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango ametembelea na kukagua mradi wa maji Same - Mwanga - Korogwe ambao umelenga kusambaza maji katika Miji ya Same na Mwanga pamoja na vijiji 38 kwenye Wilaya ya Same na Mwanga na vijiji vitano katika Wilaya ya Korogwe. 

Wakati akitembelea mradi huo ambao Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) ilipewa kazi maalum ya ulazaji wa mabomba makubwa  ya usambazaji maji, Mhe. Mpango amewaagiza watendaji wa Serikali pamoja na wakandarasi kuhakikisha wanafanya kazi usiku na mchana ili mradi uweze kukamilika kwa muda uliopangwa na wananchi waweze kupata huduma ya maji. 

"Serikali imefanya kazi kubwa kuhakikisha huduma ya maji inamfikia kila Mtanzania, hivyo niwaombe mfanye kazi ya kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya maji ifikapo Juni mwaka huu," ameeleza Mhe. Makamu wa Rais. 

Aidha Mhe. Mpango ameipongeza Wizara ya Maji kwa kutekeleza mradi huo ambao mpaka sasa umefikia asilimia 87.5 kukamilika kwake.

Katika mradi huu, DAWASA imekamilisha kazi ya ulazaji wa mabomba makubwa ya inchi 24 hadi inchi 3 kwa umbali wa kilomita 17.755 kwa Wilaya ya Same na umbali wa kilomita 54.725 kwa Wilaya ya Mwanga. 

Mamlaka imefanikiwa kutekeleza mradi huu kwa ufanisi mkubwa na sehemu kubwa ya kazi imekamilika kwa asilimia kubwa. 

Kwa upande wake Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso amemhakikishia Mhe. Makamu wa Rais kwamba Wizara ya Maji itaendelea na jitihada za kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa muda uliopangwa ili wananchi watakaohudumia na mradi huo wapate huduma ya maji ipasavyo. 

"Nikuhakikishie Mhe. Makamu wa Rais kuwa, Wizara ya Maji imejipanga na hivyo tunasimamia maagizo uliyotupa ili kuhakikisha utekelezaji wa mradi huu unakamilika," ameeleza Mhe. Aweso. 

Mradi wa maji Same Mwanga - Korogwe unatekelezwa kwa gharama ya shilingi bilioni 262 na unatarajia kuhudumia wananchi zaidi ya 400,000.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Miradi DAWASA, Mhandisi Ramadhani Mtindasi amesema kuwa Mamlaka imefanikiwa kutekeleza na kukamilisha sehemu ya mradi kwa ufanisi na kwa muda uliowekwa. 

Utekelezaji wa mradi huu ulianza mwezi Januari 2021 mara baada ya Serikali kupitia Wizara ya Maji kuikabidhi DAWASA sehemu ya mradi kutekeleza kazi ya ulazaji wa mabomba makubwa ya kusambaza Majisafi ya kuanzia inchi 24 hadi inchi 3 kwa umbali tofauti tofauti.