Wizara ya Maji

Dar es Salaam Water Supply And Sanitation Authority (DAWASA)

TIRA Logo
Mwenge wa Uhuru wapitishwa kwa kishindo mradi wa maji
11 May, 2023
Mwenge wa Uhuru wapitishwa kwa kishindo mradi wa maji

Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa Ndugu Abdalla Shaib Kaim ameridhishwa na utekelezaji wa Mradi wa Maji Mshikamano wenye thamani ya Bilioni 4.5 chini ya Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es salaam (DAWASA). 

Ndugu Kaim ameyasema hayo baada ya kukagua mradi huo  uliopo Kata ya Mshikamano Wilaya ya Ubungo leo Mei 27, 2023 na baadaye kuwasha pampu ikiashiria ukamilishwaji wa mradi huo wa kimkakati. 

Akizungumza na wananchi waliojitokeza kuupokea Mwenge Wilaya ya Ubungo,  Ndugu Kaim amesema ameridhishwa kwa asilimia mia kuanzia utekelezwaji wa mradi mzima pamoja na nyaraka muhimu zilizoambatanishwa  kwenye ukaguzi.

" Kwanza kabisa nachukua nafasi hii kumshukuru Rais wetu Mhe. Dkt Samia Suluhu kwa kuidhinisha fedha za uviko bilioni 2.5 zilizofanikisha kwa kiasi kikubwa utekelezaji wa mradi huu muhimu, Pia nawapongeza DAWASA kwa kazi iliyotukuka ya usimamizi madhubuti wa mradi huu uliondoa changamoto ya upatikanaji wa maji kwa wakazi zaidi ya 170,000 wanaoishi katika maeneo haya" amesema Ndugu Kaim

Kwa upande wake Mbunge wa jimbo la Kibamba Mhe.Issa Mtemvu amepongeza juhudi za Serikali ya awamu ya sita chini ya Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kumaliza changamoto ya maji kwa wakazi wa maeneo ya Mshikamano, Mpiji Magohe, Msakuzi Kusini, Machimbo na vitongoji vyake kwani ilikua kero ya mda mrefu hatimaye mradi umebadili historia iliyokuwepo. Ametoa wito kwa DAWASA kuhakikisha maeneo yaliyobaki yanafikiwa.

"Kwa hili nitakua mchoyo wa fadhila kama sitasema asante kwa Rais wetu, ambaye amesikia kilio cha wananchi wangu ambao kila kukicha nimekua nikiwasemea.  Hongera pia kwa DAWASA mlichokifanya kwa wakazi wa Mshikamano tuhakikishe na wengine wanafikiwa" amesema Mhe. Mtemvu

Naye, Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASA Ndugu Kiula Kingu amesema mradi wa Maji wa Mshikamano umehusisha ujenzi wa bomba kubwa la chuma la kisafirisha maji kwa umbali wa km 3, tenki lenye uwezo wa kuhifadhi lita milioni 6 na ujenzi wa kituo cha kusukuma maji. Pia ameishukuru Serikali ya awamu ya sita kwa kuendelea kuiamini DAWASA katika utekelezaji wa miradi mbalimbali na kuahidi kuendeleza kasi na ubora wa kazi ili kuhakikisha lengo la Serikali la kumtua mama ndoo kichwani linafikiwa.

"Tunaishukuru Serikali yetu kwa kuendelea kutuamini na kutuunga mkono katika kuhakikisha wananchi wote wanapata huduma ya majisafi. DAWASA itendelea kufanya kazi kwa bidii na maarifa kwa niaba ya Serikali na tutahakikisha tunawafikia wote." amesema Ndugu Kiula

Mwenge wa Uhuru 2023 uliobeba kauli mbiu "Tunza Mazingira, Okoa vyanzo vya Maji kwa ustawi wa Viumbe hai na Uchumi wa Taifa" utatembelea na kukagua miradi ya Maji inayotekelezwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es salaam (DAWASA) katika wilaya zote 5 za Mkoa wa Dar es salaam.