Wizara ya Maji

Dar es Salaam Water Supply And Sanitation Authority (DAWASA)

TIRA Logo
LIWITI KINARA MAPAMBANO UPOTEVU WA MAJI
06 Sep, 2023
LIWITI KINARA MAPAMBANO UPOTEVU WA MAJI

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es salaam ( DAWASA) kupitia mkoa wa kihuduma Tabata inaendelea na jitihada za kukabiliana na changamoto ya upotevu wa maji kwa kutekeleza mradi wa umoja unaohusisha ubadilishaji wa miundombinu chakavu na kuweka bomba mpya katika eneo la Umoja Kata ya Liwiti. 

Akizungumzia utekelezaji wa mradi huo, Mhandisi wa matengenezo Agness Mtelekesya ameeleza kuwa mradi umetekelezwa kwa awamu tatu na umehusisha ulazaji wa bomba la nchi 8 kwa umbali wa kilomita 3, na sasa upo katika awamu ya mwisho na kazi iliyobaki ni kutoa matoleo ili kuruhusu maji kuingia kwenye bomba jipya.

"Hadi sasa utekelezaji wa mradi umefika asilimia 96, na kukamilika kwa kazi hii kutamaliza changamoto ya muda mrefu ya upotevu wa maji ambayo imekua ikijirudia mara kwa mara na kusababisha adha kwa wakazi wa mtaa wa umoja," amesema Mhandisi Mtelekesya. 

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Mtaa wa Umoja Ndugu Mwaka Juma ameishukuru na kuipongeza DAWASA kwa hatua ya utekelezaji ilipofikia, na ametoa wito kwa wananchi kuwa wepesi kutoa taarifa za uharibifu wa miundombinu ya maji pamoja na kuwa mstari wa mbele kuitunza ili kuiepushia Serikali hasara ya kufanya maboresho ya mara kwa mara. 

"Napenda kuwapongeza DAWASA kwa kazi kubwa iliyofanyika bado asilimia chache mpaka kukamilika kwa mradi, kama wana umoja, tupokee funzo na nitoe wito kwa wote tutunze na kuilinda miundombinu ya maji, mbali na miundombinu kuwa chakavu lakini swala la upotevu wa maji linasababishwa na watu wachache wasio waaminifu kwa kuharibu miundombinu," amesema Mwenyekiti Juma. 

Hamida Kisena, mfanyabiashara wa mtaa wa Umoja ameipongeza Serikali kwa jitihada za kurekebisha miundombinu ya maji ambayo imekua kero kwa muda mrefu na kuchangia kusuasua kwa upatikanaji wa huduma.

"Tunaishukuru sana Serikali yetu kwa kutuondolea adha hii ambayo mbali na kuathiri upatikanaji wa maji katika eneo letu, pia uvujaji wa mabomba umepelekea uharibifu wa barabara na Mazingira kwa ujumla" ameeleza Ndugu Kisena. 

Mamlaka imeweka mikakati thabiti katika mipango yake ijayo inayokusudia kushusha kiwango cha upotevu wa maji yaani (non revenue water) kufikia kiwango cha kawaida cha upotevu wa maji kinachoruhusiwa cha asilimia 20 ikiwemo uboreshaji wa miundombinu chakavu.