Wizara ya Maji

Dar es Salaam Water Supply And Sanitation Authority (DAWASA)

TIRA Logo
KAMATI ZA KUSHUGHULIKIA MALALAMIKO WAKATI WA UTUKELEZAJI MIRADI NI TIJA KWA JAMII - UBUNGO
28 Feb, 2024
KAMATI ZA KUSHUGHULIKIA MALALAMIKO WAKATI WA UTUKELEZAJI MIRADI NI TIJA KWA JAMII - UBUNGO

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA)imezipongeza Kamati za kushughulikia malalamiko wakati wa utekelezaji wa miradi ya majisafi na usafi wa mazingira kwa kazi kubwa iliyofanyika na inayoendelea kufanyika ya kusikiliza na kutatua changamoto zinazojitokeza

Akizungumza wakati wa kikao kazi cha kuwasilisha taarifa ya kazi ya usuluhishi wa malalamiko ya wananchi wakati wa utekelezaji wa miradi, kilichohudhuriwa na wajumbe wa kamati za Ubungo na Kinondoni, Mwakilishi wa Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASA Mhandisi Modesta Mushi amesema kuwa uwepo wa Kamati zimekuwa msaada mkubwa kwa Taasisi na jamii kwa kusaidia kutoa uelewa kwa wananchi kuhusu lengo la Serikali la kutekeleza miradi hii.

Amesema kuwa ili miradi ya majisafi na usafi wa mazingira iweze kukamilika vizuri, panahitajika kamati kama hizi zinazosaidia kuwajengea uelewa wananchi juu ya hatua za utekelezaji wa mradi pamoja na ushirikishwaji wa wananchi kwenye utekelezaji wake.

Ameeleza pia kuwa kupitia kamati hizi, Mamlaka imeweza kuboresha mahusiano na wananchi wanufaika wa miradi mbalimbali ikiwemo mradi wa uondoshaji majitaka wa Mbezi Beach ambao unaendelea kutekelezwa, mradi wa ujenzi wa vituo vya huduma kwa umma ambao umekamilika, miradi ya uondoshaji majitaka pembezoni mwa mji wa Dar es Salaam na miradi ya uondoshaji majitaka kwa mfumo rahisi yenye lengo la kuboresha kuepusha uchafuzi wa Mazingira na kuboresha afya za wananchi wake.

"Mafunzo haya ni sehemu ya mkakati wa Serikali kupitia Mamlaka katika kuboresha na kuimarisha upatikanaji wa huduma ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam na Pwani, hivyo nizipongeze kamati zote kwa ushiriki wenu mzuri kwenye zoezi hili na nizidi kuwatia moyo kuendelea na nguvu hiyo hiyo kwenye miradi inayoendelea kutekelezwa," ameeleza Mhandisi Modesta.

Kwa upande wake Diwani wa kata ya Sinza ,Ndugu Raphael Awino ameipongeza Mamlaka kwa kazi kubwa inayoifanya ya kubuni na kutekeleza miradi yenye kukidhi mahitaji ya wananchi hususani miradi ya usafi wa mazingira.