KAMATI YA BUNGE YANOGESHA KILELE CHA WIKI YA MAJI KWA KUPANDA MITI DAR
Maadhimisho ya Wiki ya Maji imefika kileleni , leo Machi 22, 2024 kwa kuhusisha utekelezaji wa shughuli mbalimbali ikiwemo zoezi la kamati ya bunge ya mitaji ya umma kupanda miti ya kivuli na ya matunda katika jengo la DAWASA Yetu sambamba na uendeshaji wa dawati maalum la kusikiliza wananchi.
Maadhimisho ya Wiki ya Maji yalibeba kauli mbiu isemayo uhakika wa maji kwa amani na utulivu ambayo inaakisi jitihada kubwa za Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kumtua Mama ndoo ya maji kichwani.
Katika kuhakikisha adhma ya Mhe. Rais Samia inatimia, Serikali kupitia Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam DAWASA imetekeleza zoezi la upandaji wa miti ya kivuli na ya matunda katika jengo jipya la DAWASA Yetu kwa lengo la kutoa ujumbe kwa jamii juu ya umuhimu wa uzingatiwaji wa utunzaji wa mazingira pamoja na vyanzo vya maji ili kuweka mazingira mazuri ya upatikanaji wa huduma ya Majisafi.
Akizungumza wakati wa upandaji miti hiyo, Mwenyekiti wa Kamati hiyo Ndugu Deus Sangu amesema kuwa zoezi la upandaji miti lina umuhimu mkubwa katika kuokoa ekolojia ya upatikanaji wa maji kwenye vyanzo vya maji, na hii ni sehemu ya hatua ya kuunga mkono jitihada za Serikali za kutunza na kulinda vyanzo vya maji.
Ameongeza kuwa upandaji wa miti unatakiwa uwe utaratibu wa kila mara hususani kwenye maeneo ya vyanzo vya maji kwa lengo la kuwezesha upatikanaji wa maji.
Ameipongeza Mamlaka kwa kazi inayofanya ya kulinda na kutunza mazingira yanayowezesha katika upatikanaji wa huduma ya maji kwenye maeneo ya huduma.
Kwa upande wake Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) Ndugu Kiula Kingu amesema kuwa zoezi hili la upandaji miti limelenga kuweka msingi wa umuhimu wa uzingatiwaji wa utunzaji wa vyanzo vya maji na ulinzi wa mazingira ili kuwezesha vyanzo vya maji kuendelea kutoa maji.
Wiki ya Maji huadhimishwa mwezi Machi 16-22 ya kila mwaka kwa lengo la kuchagiza jitihada za Serikali za kukuza upatikanaji wa huduma ya Majisafi kwa wananchi ili kuhakikisha lengo la Serikali la kusambaza maji kwa wote linatimia.