Wizara ya Maji

Dar es Salaam Water Supply And Sanitation Authority (DAWASA)

TIRA Logo
JENGO JIPYA LA MAMLAKA KUONGEZA UFANISI UTOAJI WA HUDUMA - JENERALI MWAMUNYANGE
21 Nov, 2023
JENGO JIPYA LA MAMLAKA KUONGEZA UFANISI UTOAJI WA HUDUMA - JENERALI MWAMUNYANGE

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) Jenerali Mstaafu Davis Mwamunyange amesema kuwa ukamilishwaji wa jengo jipya la DAWASA yetu utachochea tija ya utoaji wa huduma ya Majisafi na Usafi wa Mazingira kwa wananchi.

Amesema hayo wakati wa ziara ya kutembelea utekelezaji wa mradi wa jengo jipya la DAWASA Yetu lililojengwa na Mamlaka kupitia Mkandarasi wa kampuni ya Uhandisi ya China (CCECC) kwa gharama ya shilingi bilioni 40.

Amebainisha kuwa ujenzi wa jengo hili umefuatia utekelezaji wa maagizo ya viongozi wa Serikali waliotutaka kupisha utekelezaji wa mradi wa reli ya kisasa ya mwendokasi.

Jenerali Mwamunyange ameongeza kuwa jengo hili ni la kisasa na litachochea kwa kiasi kikubwa utoaji wa huduma kwa ufanisi na kwa haraka hasahasa kwa kutumia mifumo ya Tehama.

"Niwapongeze wafanyakazi wa Mamlaka kwa kutekeleza kwa haraka na kwa ufanisi mkubwa zoezi la kuhamisha mali na samani kutoka kwenye ofisi za Gerezani na kuja kwenye jengo jipya la DAWASA Yetu," amesema Jenerali Mwamunyange.

"Nimefurahishwa sana na kasi ya utekelezaji wa mradi wa jengo hili na tuna matumaini kuwa mradi utaleta tija kubwa katika upatikanaji wa huduma ya majisafi na usafi wa mazingira kwa wananchi," ameeleza Jenerali Mwamunyange.

Kwa upande wake Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASA Ndugu Kiula Kingu amesema kuwa utekelezaji wa jengo hili kwa sasa umefikia asilimia 90, Mkandarasi anaendelea na kazi ili kukamilisha sehemu iliyobaki kabla ya kulikabidhi.

Amebainisha kuwa mradi huu umegharimu kiasi cha bilioni 40 na kupitia jengo hili tunategemea kuongeza tija katika utoaji wa huduma bora kwa wateja.

 

"Jengo hili litakuwa na mifumo mbalimbali ya Tehama itakayosaidia kufuatilia hali ya upatikanaji wa huduma kwenye maeneo yote ya kihuduma," amesema Ndugu Kingu.

DAWASA imehamisha baadhi ya ofisi zake ikiwemo Idara ya Fedha, Idara ya Tathmini, Ufuatiliaji na Mipango, Idara ya Uzalishaji na Usambazaji Maji, Idara ya Biashara na Kitengo cha Mawasiliano kutoka ofisi za awali zilizokuwa eneo la Gerezani (Sokoine drive)