Wizara ya Maji

Dar es Salaam Water Supply And Sanitation Authority (DAWASA)

TIRA Logo
MWANANYAMALA WAKAMILISHIWA MRADI WA USAFI WA MAZINGIRA
03 May, 2023
MWANANYAMALA WAKAMILISHIWA MRADI WA USAFI WA MAZINGIRA

MWANANYAMALA WAKAMILISHIWA MRADI WA USAFI WA MAZINGIRA

Na Fredy Mshiu

Mradi wa uboreshaji Usafi wa Mazingira Mwananyamala uliotekelezwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es salaam (DAWASA) umekamilika na sasa wananchi wameombwa kujitokeza ili kupata maunganisho mapya.

Akizungumzia utekelezaji wa mradi huo Mhandisi Gabriel Wanzagi Ameeleza kuwa mradi umekamilika kwa asilimia 100 na kazi iliyokuwa imebakia ya kuunganisha chemba za ukusanyaji Majitaka sasa imekamilika.

"Mradi huu ulioanza utekelezaji wake Oktoba 2022 umekamilika huku ikihusisha kazi ya uunganishaji wa chemba zote 32 pamoja na kazi ya kulaza mtandao wa majitaka umbali wa Km 1.6, Tunatoa wito kama Mamlaka kwa wananchi kujitokeza kwa wingi kupata maunganisho ya majitaka na kuondokana na matumizi ya mashimo ya vyoo. " ameeleza Mhandisi Wanzagi. 

Mhandisi Wanzagi ameongeza kuwa mradi huu ni muhimu kwa eneo la Mwananyamala na maeneo jirani  ambapo inaenda kusaidia Majitaka yaliyokuwa yanatirirka mtaani na kuchafua mazingira kuisha. 

Kwa upande wake mkazi wa mtaa wa Mwananyamala kanisani Ndugu Hafsa Maulid ameeleza kufurahishwa na kukamilika kwa mradi huu ambao unaleta matumaini ya usafi wa Mazingira na kuondokana na athari ya milipuko ya magonjwa.

"Mradi huu ni tiba ya tatizo la milipuko ya magojwa hususani kipindupindu na magonjwa ya kuhara unaosababishwa na utiririshaji Majitaka ovyo mtaani, kukamilika kwake sasa tunaimani kubwa Mazingira yetu yatakua safi na salama " ameeleza ndugu Maulid.

Mradi wa Usafi wa Mazingira Mwananyamala unaogharimu kiasi cha sh. Milioni 230 umehusisha ulazaji wa Bomba za kusafirisha Majitaka kwa umbali wa Km 1.6, ujenzi wa chemba 32 za kukusanya Majitaka na unategemea kuhudumia wananchi zaidi ya 100 katika mitaa ya Msufini, Barabara ya Dunga, Mwananyamala kanisani na maeneo jirani katika Kata ya Mwananyamala.