DAWASA YAWANOA MABALOZI WA USAFI WA MAZINGIRA - MKURANGA
Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam ( DAWASA) imeendeleza shughuli za kutoa elimu ya Majisafi na usafi wa mazingira kupitia klabu za Mazingira katika shule ya msingi Mkuranga iliyopo wilaya ya Mkuranga Mkoani Pwani.
Wanafunzi kutoka shule ya msingi Mkuranga wamepata fursa ya kujifunza kuhusu umuhimu wa nishati ya maji kwa maisha binadamu na viumbe hai haswa katika usafi binafsi, somo lililolenga kuwawezesha wanafunzi kufahamu vitu muhimu vya kufanya katika usafi binafsi wa mwili lakini pia njia bora za kujikinga na magonjwa ya mlipuko kama vile kuhara na matumbo.
Husna Richard, Afisa Mawasiliano msaidizi DAWASA amesema dhumuni la kutoa elimu hiyo katika ngazi ya shule ya msingi ni kutengeneza kizazi bora kinachofahamu umuhimu wa utunzaji wa mazingira na namna bora ya kufanya usafi binafsi huku maji yakiwa ni sehemu muhimu katika maisha yao.
“Usafi binafsi unatokana na mazingira yanayotuzunguka lakini pia upatikanaji wa maji ambayo ni sehemu muhimu ya usafi huo hivyo ni muhimu kuelewa na kujifunza namna bora na sahihi ya kutunza mazingira yetu na njia sahihi za kutumia maji” amesema Ndugu Husna.
Akizungumza baada ya mafunzo hayo, mwalimu Neema Minja ambae ni mlezi wa klabu ya Mazingira shuleni hapo ameishukuru DAWASA kwa jitihada za kufikia watoto wa shule za msingi na kutoa elimu ya maji na usafi wa Mazingira akiamini itakuwa chachu ya mabadiliko kwa vijana hao
“Elimu ya maji na usafi wa Mazingira ni elimu inayorithi kizazi na kizazi kwakuwa inalenga mabadiliko ya kitabia hivyo tunaishukuru sana DAWASA kwa jitihada za kutoa elimu hiyo kwa vijana wetu hakika ni adhina ya kudumu” amesema Mwl. Minja.
Ndugu. Alafa Ramadhani mwanachama wa klabu ya maji na usafi wa mazingira ya shule ya msingi Mkuranga ameishukuru Mamlaka kwa kuwa mlezi na kutoa nafasi ya wao kujifunza mambo mbalimbali ya Maji na Usafi wa Mazingira na kuomba nafasi ya kuendelea kujifunza kwa vitendo ili kufahamu zaidi namna Mamlaka inavyoendesha shughuli zake.