DAWASA YATOA MATUMAINI HUDUMA YA MAJI KWA WAKAZI WA MKURANGA
Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) imewahakikishia wakazi wa Mkuranga upatikanaji wa huduma ya maji ya uhakika baada ya kufunga transfoma mpya ya umeme itakayosaidia kusukuma maji katika chanzo cha maji eneo la Mwanambaya - Mkuranga.
Hayo yameelezwa na Afisa huduma kwa wateja wa Mkuranga Ndugu Sufian Hassan wakati wa kikao na wananchi kilichoandaliwa na Ofisi ya Kijiji cha Mipeko.
Ameeleza kuwa Mamlaka kwa kushirikiana na wadau wengine imeweza kutatua kwa kiasi kikubwa changamoto ya mgao wa huduma ya maji iliyokuwa inatokana na kukatika katika kwa umeme na wakati mwingine umeme kuwa mdogo hivyo kushindwa kusukuma maji kama inavyotakiwa, kwahiyo kwa kuweka transfoma hii inayojitegemea kunaenda kumaliza tatizo hilo.
Ndugu Sufian amewasisitiza wananchi kutumia majisafi ya DAWASA na kuacha matumizi ya maji ya kisima kwa kuwa maji yanayotolewa na Mamlaka yamepimwa na yana viwango vya ubora wa kimataifa kwa matumizi ya afya tofauti na maji ya visima, na kuwakumbusha wananchi juu ya ulipaji wa bili za maji hususani kwa wananchi wenye malimbikizo ya madeni ya maunganisho ya huduma ya majisafi ili waweze kuendelea kupata huduma bora na endelevu.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kijiji cha Mipeko A Ndugu Hamisi Mariki Mpiri ameishukuru Mamlaka kwa jinsi inavyozidi kutatua changamoto za wananchi katika upatikanaji wa huduma ya maji.
"Kila kiumbe katika hii dunia kinahitajia maji nachukua fursa hii kuwashukuru DAWASA kwa jinsi wanavyoshughulikia kero za wananchi hasa katika suala la maji," ameeleza Ndugu Mpiri.
Akiwasilisha hoja yake kwenye kikao hicho mmoja wa wananchi Ndugu Halima Yahaya ameishukuru Mamlaka kwa kutatua changamoto ya mgao wa maji na kuomba Mamlaka iwafikie wateja wengi zaidi kwani huduma ya maji ni muhimu kwa wananchi wote ili kila mmoja anufaike na kazi ya mafanikio ya Serikali.
"Pia kwa maeneo ambayo wananchi wamelipia huduma, Mamlaka ijitahidi kuongeza nguvu kusogeza huduma ili iwafikie wananchi wote," ameeleza Ndugu Halima.