DAWASA YASAFISHA MIUNDOMBINU YA MAJITAKA BUGURUNI KISIWANI
DAWASA YASAFISHA MIUNDOMBINU YA MAJITAKA BUGURUNI KISIWANI
Yasisitiza elimu utunzaji miundombinu
Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es salaam (DAWASA) imeendesha zoezi la usafishaji wa miundombinu ya majitaka katika mtaa wa Buguruni Kisiwani, Wilaya ya Ilala ikiwa na lengo la kuiongezea ufanisi na kupunguza athari za kutokea kwa magonjwa ya milipuko.
Katika eneo la Buguruni Kisiwani ,DAWASA imetekeleza mfumo rahisi wa uondoshaji majitaka majumbani ujulikanao kama Simplified Sewerage System ambao unatajwa kuwa wakisasa na unaopunguza gharama za uondoshaji majitaka kwa wananchi wa kipato cha chini.
Kupitia zoezi hili, DAWASA imebaini matumizi yasiyo rafiki ya miundombinu ya majitaka ambapo wananchi wamekua na tabia ya kutupa taka ngumu katika miundombinu hiyo kama vile nguo kukuu, taulo za watoto na kusababisha miundombinu kuzidiwa.
Mwenyekiti wa mtaa wa Buguruni Kisiwani Uwesu Bakari Uwesu ameshukuru jitihada zilizofanywa na DAWASA za kusafisha miundombinu ya majitaka na kuleta ahueni kwa wakazi wa maeneo hayo ambao walikuwa na wasiwasi wa kutokea kwa magonjwa ya mlipuko.
"Ushirikiano kati ya DAWASA na Serikali ya mtaa ni wakuridhisha, wamekua wepesi kutatua kero zinapotokea na kipekee tunashukuru kwa wao kufika mtaani hapa kusafisha miundombinu hii ya majitaka ambapo baadhi ilianza kuziba na kutiririsha majitaka mtaani" ameeleza ndugu Uwesu.