DAWASA YAPONGEZWA USIMAMIZI MZURI HUDUMA KWA WATEJA
Baraza la ushauri la Watumiaji wa huduma za Nishati na Maji (EWURA CCC) imeipongeza Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) kwa kuwa na mfumo mzuri wa utoaji wa huduma za majisafi na usafi wa mazingira kwa wateja.
Hayo yameelezwa na Afisa huduma kwa wateja kutoka EWURA CCC Ndugu Catherine Ochido wakati wa kikao kazi cha kubadilishana uzoefu wa namna EWURA CCC wanavyofanya kazi ya kusimamia haki ya wateja pamoja na Mamlaka za Majk kupitia utekelezaji wa miradi ya majisafi na usafi wa mazingira.
Ameeleza kuwa EWURA CCC imeona kazi kubwa ambayo DAWASA inafanya ya kutoa huduma kwa ufanisi na kwa kuzingatia viwango vya ubora hususani katika kumjali na kumsikiliza mteja.
“Tumejifunza namna Mamlaka inavyoshughulika na changamoto za bili za maji, huduma ya maji ya maunganisho mapya, usomaji wa mita, namna wanavyomshirikisha mteja katika zoezi zima la usomaji mita pamoja na maunganisho ya maji kwa kutumia mita mpya na za kisasa za malipo kabla (prepaid meters),” ameeleza.
Amesema pia kuwa kwa huduma za majisafi pia Mamlaka imeweka utaratibu mzuri wa uondoshaji na ukusanyaji wa majitaka toka majumbani ambayo yanakusanywa kwenye mabwawa na mengine kuchakatwa kwenye mitambo ya kisasa.
Kwa upande wake Meneja wa huduma kwa wateja DAWASA , Ndugu Doreen Kiwango amesema kuwa kikao hiki kililenga kubadilishana uzoefu wa namna bora ya kuboresha utoaji wa huduma kwa wateja kwa ufanisi.
Ameongeza kuwa Mamlaka imefanikiwa kuanza zoezi la ufungaji wa mita za maji za kisasa za lipa kabla, ikiwa ni sehemu ya maagizo ya Serikali ya kufunga mita hizi ili kuongeza ufanisi katika utoaji huduma.
Ameeleza kuwa kwa sasa mita hizi za kisasa kwa majaribio kwenye eneo la nyumba za viongozi Mikocheni na Victoria,.
“Tunategemea kufunga mita hizi za lipa kabla katika maeneo mengine ya Kinondoni, Tegeta na Makongo ambako tayari pameshafanyiwa tathmini,” ameeleza.
Mbali na hapo, ujumbe wa EWURA CCC walipata nafasi ya kutembelea na kujifunza namna mabwawa ya kuhifadhi majitaka yanavyofanya kazi pamoja na mitambo ya kuchakata majitaka inavyosaidia kuboresha usafi wa mazingira kwenye makazi ya watu.