Wizara ya Maji

Dar es Salaam Water Supply And Sanitation Authority (DAWASA)

TIRA Logo
DAWASA YAHAMASISHA ULIPAJI ANKARA KWA WAKATI UBUNGO
06 Sep, 2023
DAWASA YAHAMASISHA ULIPAJI ANKARA KWA WAKATI UBUNGO

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) imetoa elimu ya umuhimu wa kufanya malipo ya huduma ya maji kwa wakati, maunganisho mapya ya maji, na utunzaji wa miundombinu ya maji kwa wakazi wa eneo la Matosa Kata ya Goba, Wilaya ya Ubungo.

Akizungumza wakati wa zoezi la nyumba kwa nyumba, Mwenyekiti wa Mtaa wa Matosa Halisi Ndugu Ramadhani Jacob Masele ameipongeza Serikali kupitia DAWASA kwa utekelezaji wa mradi wa maji Makongo Bagamoyo kwani umetatua changamoto ya ukosefu wa maji iliyodumu kwa muda mrefu katika eneo hilo. Pia ameipongeza Mamlaka kwa kufanya jitihada za kuendelea kutoa elimu kuhusu huduma zinazotolewa na kutatua changamoto zinazojitokeza kwa wakati.

“Napongeza jitihada za DAWASA za utoaji wa elimu, ambayo itasaidia kufahamu taratibu rasmi za kupata huduma, njia za kulipa ankara za maji na umuhimu wa kulipa kwa wakati lakini pia tumekumbushwa kutunza miundombinu ya maji ili kuendelea kufaidi huduma ya maji,” ameeleza Ndugu Ramadhani.

Afisa Biashara Mkoa wa Kihuduma DAWASA Makongo Ndugu Rita Mgumira ameeleza kuwa utoaji wa elimu ya malipo ya huduma ya maji kwa wakati imesaidia kuhamasisha wananchi na kuongeza muitikio wa ulipaji wa huduma hizo kwa wakati bila usumbufu. Hali hii imeongeza ari na kuhakikisha huduma ya maji inayotolewa ni bora na ya uhakika.

Ameongeza kwa kusema elimu ya uhamasishaji ulipaji wa madeni, utunzaji wa miundombinu ya maji pamoja na taratibu rasmi za kupata huduma inayotolewa na Mamlaka inasaidia kuepusha ubadhilifu kwa kuwa wananchi wanakuwa na taarifa sahihi kutoka kwa Mamlaka.

“Zoezi la kupita nyumba kwa nyumba kutoa elimu limekuwa utamaduni wetu kwa sasa kwani linasaidia kujenga mahusiano ya karibu na wateja tunao wahudumia, kutatua changamoto zao za Kihuduma kwa haraka na kuboresha huduma tunazoazitoa. Zoezi hili ni endelevu ili kuhahikisha wateja wanaridhika na huduma tunazotoa, lakini pia kutimiza dira kuu ya Mamlaka ambayo ni kutoa huduma za majisafi na usafi wa mazingira zenye ubora wa viwango vya juu kwa ustawi na maendeleo ya jamii,” ameeleza Ndugu Rita.   

Nae mkazi wa Matosa Mtaa wa Halisi Ndugu Hadija Iddi ameeleza furaha yake na kuishukuru Mamlaka kwa kutekeleza mradi ambao umeondoa adha ya kukosa huduma ya maji kwa muda mrefu.

“Naishukuru Serikali kwa kutambua adha ya muda mrefu waliyokuwa wanaipata wananchi wa Matosa, kwani kupitia mradi huu mkubwa kilio cha maji kwa sasa kwetu kimekuwa historia. DAWASA wamekuwa mstari wa mbele kuhakikisha tunapata huduma bora na kupitia hii elimu wanayoitoa nyumba kwa nyumba, hakika tutalipa madeni yetu kwa wakati ili tuendelee kufurahia huduma," ameeleza Ndugu Hadija.