Wizara ya Maji

Dar es Salaam Water Supply And Sanitation Authority (DAWASA)

TIRA Logo
DAWASA YAGONGA HODI KWA WANANCHI MAKONGO WIKI YA HUDUMA KWA WATEJA
09 Oct, 2023
DAWASA YAGONGA HODI KWA WANANCHI MAKONGO WIKI YA HUDUMA KWA WATEJA

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es salaam (DAWASA) imeadhimisha wiki ya huduma kwa wateja kwa kutembela wateja wakubwa na wadogo katika eneo la Makongo Jijini Dar es salaam.

Akizungumza na  wateja mbalimbali, Mkurugenzi wa Biashara (DAWASA) CPA (T) Rithamary Lwabulinda ameahidi kuendelezaa  ushirikiano baina ya Mamlaka na wateja wake ili kuhakikisha huduma bora inawafikia wote kwa wakati.

"Kwa Chuo Cha Ardhi tunatekeleza mradi wa kuongeza huduma ya maji utakaosaidia ujenzi wa majengo ya chuo na ifikapo tarehe 7, Oktoba 2023 huduma ya maji itakua imeanza imefika eneo la ujenzi" ameeleza ndugu Lwabulinda.

Lwabulinda ameongeza kuwa  Mamlaka imejipanga kuongeza maunganisho ya huduma ya maji na kufikia asilimia 95 ya upatikanaji wa huduma ifikapo mwaka 2025.

"Tumeadhimisha wiki ya huduma kwa wateja kwa kutembelea wateja wetu wakubwa na wadogo, tunafahamu Kuna maeneo ambayo bado huduma haijafika, nipende kuwahakikishia Mamlaka inafanya kazi kubwa kusogeza huduma maeneo yote kwa kuongeza vyamzo vya maji na kufanya miradi ili kila mwananchi apate huduma ya maji" ameeleza ndugu Lwabulinda.

Makamu Mkuu wa Chuo cha Ardhi Profesa Evaristo Liwa ameishukuru DAWASA kwa huduma Bora wanazowapatia chuoni hapo na kuahidi ushirikiano wa kutosha baina ya chuo na DAWASA.

"Nikiri kwamba DAWASA wanatoa huduma bora hapa kwetu, huduma ya maji tunaipata kama inavyostahiki  na imechangia utulivu mkubwa kwa wanafunzi chuoni hapa, tutaendelea  kutoa ushirikiano kwao Ili huduma hii bora iwe endelevu" ameeleza Profesa Liwa.

Kwa upande wake ndugu Frida Jackson mkazi wa Makongo ameishukuru DAWASA kwa kuwatembelea na kueleza furaha yake Kwa huduma bora wanazopata.

"Miaka ya nyuma Makongo tulikua na shida kubwa ya maji, lakini sasa huduma imeimarika sana, tunapata huduma masaa 24, nitumie nafasi hii kuwahasa wananchi wenzangu kulipia huduma za maji kwa wakati ili na sisi tuweze kupata huduma bora kwa wakati"ameeleza ndugu Frida.

Wiki ya huduma kwa wateja inaakisi huduma bora zinazoendelea kutolewa na Mamlaka kwa wateja wake wote huku ikibeba kauli mbiu inayosema "Huduma kwa Ushirikiano".