DAWASA YABORESHA UTOAJI HUDUMA KITUO CHA AFYA CHANIKA
DAWASA YABORESHA UTOAJI HUDUMA KITUO CHA AFYA CHANIKA
Na Crispin Gerald
Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) Kisarawe inatekeleza mradi mkubwa wa kusambaza majisafi katika kituo cha afya Chanika, kilichopo Wilaya ya Ilala, Dar es Salaam.
Mradi huu ni muhimu kwa lengo la kuboresha na kurahisisha utoaji wa huduma za afya kwa wananchi wengi wanaohudumiwa kwenye kituo hicho cha Chanika.
Akizungumza kuhusu utekelezaji wa mradi huu Msimamizi wa mradi Mhandisi Erasto Mwakilulele amesema kuwa hii ni kazi muhimu kwa kuwa inalenga kusaidia upatikanaji wa maji kwenye kituo hiki ambacho kwa muda mrefu wauguzi wamekuwa wakitumia maji ya chumvi.
"Tumeona haja ya kutekeleza mradi huu wa kupeleka huduma kwenye Hospitali kutokana na uhitaji mkubwa wa maji uliopo kwenye kituo hiki cha ya afya kinachohudumia wakazi wengi wa Wilaya ya Ilala, Mamlaka inatambua kuwa huduma ya majisafi ni muhimu sana katika utoaji wa huduma ya afya," ameeleza Mhandisi Mwakilulele.
Amesema kuwa utekelezaji wa mradi umehusisha ulazaji wa mabomba makubwa ya inchi 4, 3 na 2 kwa umbali wa kilomita 1550 kwenda kwenye Hospitali hiyo.
"Mradi huu tunautekeleza kwa kutumia chanzo cha maji cha tenki la Kisarawe lenye ujazo wa lita milioni 6, ambalo litasambaza maji kwa msukumo mkubwa kwenda hospitali," ameeleza Mhandisi.
Sambamba na hilo, mradi utanufaisha pia wakazi wa mitaa mbalimbali inayopitiwa na mradi, ambapo jumla ya kaya 200 za mitaa ya Nyeburu, Nguvu mpya na barabara ya Kilimahewa itanufaika.
"Mpaka sasa tumeweza kutekeleza mradi huu kwa asilimia 85, ambapo mwisho wa mwezi wa sita huduma katika hospitali ya Chanika itaanza kupatikana.
Kwa upande wake Mganga Mfawidhi wa kituo cha Afya Chanika Ndugu Pascal Nkii amesema kuwa ukosefu wa huduma ya maji umekuwa ukisababisha matumizi makubwa ya fedha kwa lengo la kupata majisafi kituoni.
Amesema pia ukosefu wa maji unaathiri uendeshaji wa mitambo ya afya hivyo kulazimika kutumia gharama kubwa ya kununua maji,
Amesema kwa wastani kituo hicho hupokea wagonjwa 750 kwa siku, hivyo huwa panakuwa na changamoto hasa wakati wa kuhudumia wagonjwa bila majisafi. Mradi huu wa maji utakuwa mkombozi mkubwa sana kwetu.
Mwajuma Shomari mkazi wa Chanika aliyepata huduma hospitali ya Chanika ameipongeza DAWASA kwa kuondoa changamoto ya ukosefu wa maji kwenye hospitali yao, maana wamekuwa wakitumia maji ya chumvi kwa muda mrefu ambayo sio salama kiafya.
Amebainisha kuwa huduma ya majisafi kwenye hospitali ni ya muhimu sana hasa kwa huduma ya Mama na mtoto.
Amesema kuwa huduma ya majisafi itawasaidia sana wamama na watoto wakati wa huduma za afya.