DAWASA NA BONDE LA WAMI RUVU WANOGESHA WIKI YA MAJI KWA KUPANDA MITI MAENEO YA MTO RUVU
Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) kwa kushirikiana na Bonde la Wami Ruvu imeshiriki zoezi la upandaji miti katika Shule ya Sekondari Ruvu Station iliyopo kijiji cha Ruvu Station Kata ya Ruvu Wilaya ya Kibaha na maeneo yanayozunguka mto Ruvu.
Zoezi hili limeambatana na utoaji wa elimu ya uhifadhi wa Mazingira kwa Wanafunzi wa Shule ya Sekondari Ruvu Station na wananchi wanaoishi maeneo ya jirani na mto Ruvu juu ya uharibifu wa vyanzo vya Maji utokanao na mabadiliko ya tabia nchi na shughuli za kibinadamu, ambapo miti zaidi ya 300 imepandwa katika eneo hilo la shule na maeneo ya jirani ya mto Ruvu.
Katika muendelezo wa kuadhimisha wiki ya maji Nchini , Mamlaka na Bonde la Wami Ruvu inaendelea na zoezi la kulinda na kutunza vyanzo vya maji na mazingira kwa ujumla ili kuleta ustawi wa viumbe hai .
Mamlaka inaamini upatikanaji wa maji unategemea sana jitihada za makusudi zinazofanywa na wadau mbalimbali katika kulinda mazingira kuanzia kwenye milima inayotoa maji na mito inayosafirisha maji hayo hadi kufika kwa mtumiaji wa mwisho.
DAWASA katika kipindi hiki cha maadhimisho ya wiki ya maji ambayo huadhimishwa kila mwaka tarehe 16-22 Machi imeshirikiana na viongozi wa vijiji, wakulima na wafugaji wa maeneo ya Minazimikinda, Ruvu station, Lubungo, Kitomondo na vijiji vilivyo kando kando ya mto Ruvu kupanda miti kwa lengo la kutunza na kulinda mazingira yanayozunguka Mto Ruvu ili kuokoa uharibifu wa chanzo hiki cha maji.
Maadhimisho ya wiki ya Maji mwaka 2024 yamebeba kauli mbiu "Uhakika wa maji kwa amani na utulivu"