CHINA YAAHIDI KUONGEZA NGUVU MKAKATI KUMTUA MAMA NDOO YA MAJI KICHWANI
CHINA YAAHIDI KUONGEZA NGUVU MKAKATI KUMTUA MAMA NDOO YA MAJI KICHWANI
Na Crispin Gerald
Balozi wa China nchini ameahidi kuendelea kishirikiana na serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika mikakati ya uboreshaji wa huduma za majisafi na usafi wa mazingira.
Akizungumza baada ya ziara ya kutembelea na kukagua mtambo wa Wami, Balozi wa China Mhe. Chen Mingjian amesema anafurahi kuona kazi kubwa ambayo imefanyika katika kuongeza uzalishaji wa maji kutoka katika mtambo huo wa maji ambao ulijengwa kwa ushirikiano kati ya Serikali ya Tanzania na China.
Ameongeza kuwa Serikali ya China ipo tayari kuendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika kuboresha miundombinu katika mtambo wa Wami ili uweze kutoa huduma bora zaidi kwa wananchi inaowahudumia.
"Tunaipongeza DAWASA kwa hatua ilizozichukua za kutunza na kuboresha miundombinu pamoja na kufanya upanuzi wa mtambo, hizi ni jitihada kubwa za kupongezwa, kwa kuwa zinalenga kutoa huduma kwa wananchi wengi," amesema Balozi Chen.
Akitoa maelezo kwa Balozi kuhusu chanzo hicho muhimu cha maji, Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASA Bw. Kiula Kingu amesema kuwa ziara ya Mhe. Balozi wa China imelenga kufuatilia maendeleo ya mtambo huo ulizinduliwa rasmi mwaka 2001.
Amebainisha kuwa nia ya ziara hiyo fupi ilikuwa ni kutembelea mifumo ilihojengwa hapo awali na baadaye kujadili maeneo muhimu ya ushirikiano kwa lengo la kukuza mahusiano baina ya mataifa haya mawili rafiki.
Serikali kwa kushirikiana na Benki ya Exim India, imefanya maboresho ya upanuzi wa uzalishaji wa mtambo wa maji kutoka lita milioni 7.2 mpaka lita milioni 21 kwa sasa na kuweza kuhudumia wananchi 197,000 na vijiji 47.
"Mpaka sasa utekelezaji wa mradi wa Chalinze awamu ya tatu umefikia asilimia 95" alisema na kuongeza kuwa kazi iliyobaki ni kuweka mifumo ya tehama ili kuweza kusimamia miundombinu ya mradi huu wenye kugusa mikoa ya Pwani na maeneo ya mikoa ya Morogoro na Tanga.
"Mifumo hii itaiwezesha DAWASA kufuatilia mwenendo wa ujazaji maji katika matenki na usambazaji maji," ameeleza Ndugu Kingu.
"Lengo la maboresho haya ni kuhakikisha tunakuza upatikanaji wa maji kwenye maeneo ya mijini na vijijini yanayohudumiwa na mradi huu kwa asilimia 95 mijini na 85 vijijini," ameongeza.
Kwa upande wake Bi Mwajuma Saidi mkazi wa Msata ameishukuru Serikali kupitia DAWASA kwa kuwatua ndoo kichwani wakazi wote wa eneo lao.
"Kero ya maji ilikuwa kubwa kwenye eneo hili, tulikuwa tunafuata maji bondeni yenye chumvi ambayo hayakuwa salama kiafya, kwa sasa tunashukuru shida imeisha," ameeleza.
Mradi wa maji Chalinze awamu ya tatu umetekelezwa na DAWASA kwa lengo la kutoa huduma kwa wananchi 274,603 wa mji wa Chalinze, Morogoro, Pwani, Ngerengere na baadhi ya vijiji vya Wilaya ya Handeni, Mkoani Tanga.