Wizara ya Maji

Dar es Salaam Water Supply And Sanitation Authority (DAWASA)

TIRA Logo
CCM KIBAHA YACHAGIZA UTEKELEZAJI WA MRADI WA MAJI PANGANI
15 Sep, 2023
CCM KIBAHA YACHAGIZA UTEKELEZAJI WA MRADI WA MAJI PANGANI

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA), imeanza mchakato wa ujenzi wa mradi wa maji Pangani kwa lengo la kufikisha huduma ya majisafi kwa wananchi wa Kata ya Pangani, Mji wa Kibaha, Mkoa wa Pwani.

Akizungumzia maandalizi ya mradi huu Meneja wa Mkoa wa Kihuduma DAWASA Kibaha Ndugu Alpha Ambokile amebainisha hayo wakati wa ziara ya Kamati ya Siasa ya Wilaya iliyotembelea eneo ambalo mradi huo unaenda kutekelezwa.

Amesema kwamba mradi huu utatekelezwa kwa gharama ya bilioni 9.8 ambazo ni fedha za Serikali, na utatekelezwa kwa muda wa miezi kumi na nane baada ya kusaini hati ya makubaliano baina ya mkandarasi na DAWASA yanayotarajiwa kusainiwa mwishoni mwa mwezi Septemba.

"Tayari mkandarasi wa mradi amepatikana na sasa ni wakati wa kusaini hati ya makubaliano ili utekelezaji wa mradi uanze rasmi na tunaamini ndani ya miezi kumi na nane kazi itakuwa imekamilika," amesema Ambokile.

Ameongeza kuwa mradi huu utatekelezwa kwa awamu mbili, ambapo awamu ya kwanza itahusisha ujenzi wa nyumba ya mitambo (pump house), tank dogo la kutunza na kusafirisha maji (swap tank) la lita milioni moja, tenki la kuhifadhi maji la lita milioni sita, bomba kuu la inchi 12 la kusafirisha maji kutoka kwenye chanzo cha Mtambo wa Ruvu Juu mpaka kwenye tenki kwa umbali wa kilomita 14 na bomba kuu la kusafirisha maji kwa wateja kwa umbali wa kilomita 4.

Mradi unalenga kunufaisha wakazi 30,000 wa Kata ya Pangani mji wa Kibaha, Mkoa wa Pwani.

Akizungumzia utekelezaji wa mradi huu, Mwenyekiti wa Kamati ya Siasa Ndugu Mwajuma Nyamsa ameiomba Mamlaka iongeze bidii ya utekelezaji wa mradi huo ili wananchi wa mji huu waondokane na adha ya maji.

"Wananchi wa maeneo haya ya Pangani wamekuwa kwenye shida ya maji kwa muda mrefu, kutokana na kutokwepo na miundombinu ya majisafi, hivyo kupitia mradi huu, wananchi watanufaika kikamilifu," ameeleza.

Niwaombe DAWASA kuongeza nguvu zaidi ili mradi huo utekelezwe kwa wakati na kuwaondolea wananchi adha ya maji," ameongeza Ndugu Mwajuma.

Mradi wa Maji Pangani ni mojawapo ya mradi wa kimkakati unaotekelezwa na DAWASA kwa kushirikiana na Serikali kwa lengo la kuimarisha upatikanaji wa huduma ya Majisafi kwa wananchi wote.