Wizara ya Maji

Dar es Salaam Water Supply And Sanitation Authority (DAWASA)

TIRA Logo
BOKO MNEMELA WAHAKIKISHIWA UBORESHAJI WA HUDUMA
05 Sep, 2023
BOKO MNEMELA WAHAKIKISHIWA UBORESHAJI WA HUDUMA

Katika kuhakikisha huduma ya majisafi inawafikia wananchi wote kwenye eneo lake la kihuduma, Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es salaam (DAWASA) inaendelea na utekelezaji wa mradi wa Boko Mnemela katika kata ya Boko Mnemela Wilaya ya Kibaha, Mkoa wa Pwani ambao utekelezaji wake umefikia asilimia zaidi ya 40.

Akizungumzia maendeleo ya utekelezaji wa mradi huo, msimamizi wa mradi Mhandisi Charles Stephen amesema utekelezaji wa mradi umehusisha ulazaji wa bomba za nchi 3,4,6,8 na 12 kwa umbali wa kilomita 4 kati ya kilomita 10 zinazotegemewa  kufikiwa ili kukamilisha mradi.

"Mradi unaendelea kutekelezwa kwa kasi na tupo kwenye hatua nzuri kwani kwa maeneo ambayo tayari bomba limepita wameanza kunufaika na huduma ya majisafi na tuna uhakika kukamilika kwa mradi kutaenda kumaliza changamoto iliyopo ya huduma kwa mda mrefu" amesema Mhandisi Stephen

Mhandisi Stephen ameeleza mradi umetokana na changamoto ya ongezeko la wakazi hivyo mahitaji kuzidi uwezo wa miundombinu na uchakavu wa miundombinu iliyoshindwa kupeleka maji kwa msukumo mkubwa kwenye kata ya Boko Mnemela na viunga vyake.

Mradi wa maji Boko Mnemela unatekelezwa kwa gharama ya zaidi ya Milioni 170 na unategemewa kuhudumia wakazi  takribani 1,500 wa maeneo ya Boko Mnemela, Boko Temboni, Mwanalugali, Timiza, Tumbi na Shirika la elimu la Kibaha.