Wizara ya Maji

Dar es Salaam Water Supply And Sanitation Authority (DAWASA)

TIRA Logo
BARAZA LA WAFANYAKAZI DAWASA WAADHIMIA KUMTUA MAMA NDOO KICHWANI 
28 Feb, 2024
BARAZA LA WAFANYAKAZI DAWASA WAADHIMIA KUMTUA MAMA NDOO KICHWANI 

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) imefanya mkutano wake wa pili wa Baraza kuu la wafanyakazi kwa lengo la kujadili, kutafakari na kutoa suluhu kwa changamoto zinazowakabili watumishi pamoja na uboreshaji wa huduma za maji na usafi wa Mazingira katika mikoa ya Dar es Salaam na Pwani.

Hayo yamebainishwa na Mwenyekiti wa Baraza kuu la wafanyakazi DAWASA ambae pia ni Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASA, Ndugu Kiula Kingu  wakati akifungua kikao kazi na wajumbe wa Baraza hilo ambapo ameeleza kuwa lengo kuu ni kuboresha maslahi ya watumishi ili kuongeza morali ya utendaji  na kufanikisha adhma ya Serikali ya awamu ya sita ya kumtua mama ndoo ya maji kichwani.

"Ndugu wajumbe wenzangu leo tumekutana tujadili na tufikirie  namna bora na nzuri kwa Mamlaka yetu tunaweza kuivusha ili iweze iongeze kasi katika kutoa huduma za majisafi na usafi wa mazingira kwa ufanisi zaidi" Alisema Ndugu Kingu.

"Lengo la Serikali ni kufikia asilimia 95 ya upatikanaji wa huduma ya Majisafi mjini ambapo kwa sasa tuko asilimia 93, nina imani kupitia maarifa na juhudi kubwa za wajumbe wa baraza hili tutafanikiwa kukamilisha hizo asilimia 2 zilizobaki katika mwaka wa fedha 2024/2025 na kufikia lengo lilowekwa" alisema Ndugu Kingu.

Utekelezaji wa vikao kazi vya mabaraza ya wafanyakazi ni takwa la kisheria ambapo lengo kuu ni kudumisha umoja mahala pa kazi pamoja na kushirikishana mipango iliyopo na utekelezaji majukumu kwa wafanyakazi wa kada mbalimbali.