AGIZO LA MHE RAIS SAMIA KWA WATEJA HUDUMA BILA FAINI DAWASA WAANZA UTEKELEZAJI
Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) imeanza utekelezaji wa agizo la Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso la kuwarudishia huduma ya maji wateja waliositishiwa huduma kwa msamaha wa kutolipa pesa ya faini ya kurudishiwa huduma alilolitoa mapema wiki hii kwenye vyombo vya habari.
Mhe Aweso amesema kuwa agizo hilo limetolewa na Mhe Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt Samia Suluhu Hassani katika salamu za kilele cha wiki ya Maji kwa kuagiza kuondoa faini na msamaha kwa kipindi cha mwezi mmoja huku mteja akiwajibika kulipa sehemu ya deni lake tu.
Akizungumza wakati wa utekelezaji wa Agizo katika baadhi ya maeneo ya Jiji la Dar es salaam, Bi. Maria Sanga mkazi wa Kijiji cha Wavuvi, Kata ya Kurasini amesema "nyumbani kwangu tulisitishiwa huduma ya maji kwa miaka mingi sababu ya deni kubwa tukashindwa kulipa bili, tumeteseka muda mrefu bila ya maji ya uhakika lakini tunamshukuru sana Mhe. Rais Mama Samia kupitia Waziri wa Maji, kwa kutoa msamaha wa faini ya kurudishiwa maji bila ya faini pamoja na kuturuhusu kulipa deni kidogo kidogo huku tukiendelea kufurahia huduma ya maji" aliongeza
Kwa upande wake , ndugu Sarah Herman mkazi wa Kata ya Yombo amesema "Maisha ya sasa ni magumu, tulisitishiwa huduma ya maji sababu ya kulimbikiza malipo ya bili za maji lakini jana tulipunguza deni na leo tumeona DAWASA wamekuja kurudisha maji bure bila ya kulipa faini, hii imetusaidia kuokoa pesa na kusaidia kufanya matumizi mengine ya kujikimu na maisha" Ameeleza Bi. Sarah.
DAWASA inaendelea kuwahimiza na kuwakaribisha wateja wote waliositishiwa huduma ya maji kwa sababu ya kutolipa ankara zao wafike katika ofisi za Mikoa ya Kihuduma iliyokaribu nao ili kuweza kuweka makubaliano ya malipo ya madeni hayo na waendelee kufurahia huduma ya maji.
Msamaha huu wa kutolipa faini ya kurudishiwa huduma ya Maji itakuwepo kwa muda wa siku 30 kuanzia mwezi Machi hadi Aprili, 2024 kwa Mamlaka za Maji Nchini.