27 Oct, 2021
KIWANDA CHA SUKARI CHA KILOMBERO KUPANUA UWEKEZAJI WAO KWA KUJENGA KIWANDA KINGINE NCHINI
KIWANDA CHA SUKARI CHA KILOMBERO KUPANUA UWEKEZAJI WAO KWA KUJENGA KIWANDA KINGINE NCHINI
Serikali katika kuboresha mazingira ya biashara/uwekezaji nchini, yanazidi kuonekana. Hii ni kufuatia kampuni ya uzalishaji wa Sukari ya Kilombero kukubali kutumia zaidi ya shilingi bilioni 584 za kitanzania kutokana na faida zake kuziwekeza tena nchini kwa ajili ya upanuzi/ ujenzi wa kiwanda kingine cha sukari Mkoani Morogoro.
Katika uwekezaji, maamuzi ya aina hiyo yana maana kubwa kwani mwekezaji alikuwa na uwezo wa kutumia fedha hiyo kwenda kuwekeza sehemu/ nchi nyingine. Ujenzi huo unatarajiwa kuanza Mwezi Mei Mwaka huu baada ya taratibu zote kukamilika.
Kampuni hiyo ambayo inatumia mfumo wa kuwajumuisha Wakulima wadogo wadogo, kwa sasa inafanya na wakulima elfu 6,600 wa zao la miwa na wanazalisha kati ya tani 550,000 mpaka 600,000 kwa mwaka na wanalipwa kati ya shilingi bilioni 60-65 za kitanzania kwa msimu.
Bw. Guy Williams Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Kilombero amezungumza wakati wa ziara ya Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania TIC Dkt. Maduhu Kazi na Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Sukari Profesa Kenneth Kitundu kwamba lengo la upanuzi huo wa kiwanda ni kuongeza uzalishaji wa sukari nchini.
“Tunategemea kujenga kiwanda hiki kuanzia Mei 2021 na kitazalisha tani 139,000 za sukari kiasi ambacho kitapunguza uhaba wa sukari nchini katika mwelekeo wa nchi kujitosheleza ifikapo 2025 na pia kuchangia kupunguza fedha ya Serikali inayotumika kuagiza sukari nje ya nchi kiasi kinachokadiriwa kuwa Tsh Bilioni 170 kwa mwaka.
Aidha, mradi huo unategemea kuzalisha umeme kwa matumizi ya kiwandani na zaidi ya MW10 zinaweza kwenda kwenye gridi ya Taifa.Kiwanda kitakuwa ni kikubwa Kusini mwa Afrika Mashariki kwa miaka 40 iliyopita na kitasaidia kuwapo ongezeko la mchango wa kiwanda cha Kilombero kwenye uchumi wa Tanzania kutoka Tsh 340 Bilioni -770 Bilioni kwa mwaka” amesema Bw. Guy Williams.
Kwa pamoja viongozi hao wamefurahia maboresho yanayofanywa na kampuni hiyo katika kuinua uchumi na pia kutatua upungufu wa sukari nchini na wameahidi kushirikiana nao katika hatua za utekelezaj mradi.

