HOTUBA YA MHE. MKUU WA MKOA WA DAR ES SALAAM KATIKA UFUNGUZI WA MKUTANO WA WADAU KUTOA MAONI YA NAULI ZA MABASI
Tarehe: 13 Aprili 2022
Mahala: Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Julius Nyerere Dar es Salaam
- Ndugu Mkurugenzi Mkuu wa LATRA, Gilliard Ngewe
- Ndugu Wakuu na wawakilishi wa taasisi mbalimbali za Serikali
- Ndugu wasafirishaji, Chama cha Wamiliki wa mabasi (TABOA), TATOA na DACOBOA
- Ndugu Kaimu Katibu Mtendaji wa Baraza la Ushauri la
- Huduma za Usafiri Ardhini,
- Chama cha Kutetea Abiria,
- Ndugu wadau mbalimbali mliojumuika hapa
- Ndugu wanahabari,
Wageni waalika mabibi na mabwana
Awali ya yote, namshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa Rehema kwa kuendelea kutupa uhai na kuibariki Serikali yetu, chini ya uongozi mahiri wa Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Pia nashukuru kwa heshima niliyopewa na LATRA ya kuwa mgeni Rasmi katika ufunguzi wa mkutano huu wa wadau unaolenga kupokea maoni kuhusu nauli za mabasi nchini.
Ndugu wageni waalikwa,
Nafahamu kuwa moja kati ya misingi ya utawala bora ni ushirikishwaji, nasi kama wadau kwa upande wa Serikali tunafurahi kushuhudia wadau wakishiriki kikamilifu na kwa idadi kubwa kiasi hiki kutoa maoni yao kabla ya maamuzi kufanyika.
Aidha, nakubaliana na kauli ya Mkurugenzi Mkuu wa LATRA kuwa huduma ya usafiri ni huduma ya lazima katika jamii. Hivyo napenda kutoa wito kwetu wadau tuwe mabalozi wa dhati, katika kujadili kwa hoja zenye mashiko bila jazba.
Ndugu wageni waalikwa,
Kwa kuwa jukumu hili tunalofanya leo, la kujadili na kutoa maoni juu ya nauli za mabasi nchini, ni kwa mujibu wa Sheria, nawasihi kila mmoja wetu, kwa kuzingatia umuhimu wa kazi hii atimize wajibu wake kwa umahiri na utulivu wa hali ya juu.
Pia, nimefurahi kusikia Mkurugenzi Mkuu wa LATRA amesema kuwa wadau ambao hawakuweza kufika hapa wanaweza kuendelea kuwasilisha maoni yao kwa maandishi hadi tarehe 27 mwezi Aprili mwaka huu.
Natoa rai kwa wadau mbalimbali kuitumia vizuri nafasi hii, ili kuwawezesha wataalamu wetu wafanye kazi yao kwa ufanisi wa hali ya juu.
Ndugu wageni waalikwa,
Napenda kutumia fursa hii kuwakumbusha watanzania mnaonisikia hapa na popote mlipo kupitia vyombo vya habari kuwa tushiriki kikamilifu katika kuwezesha anwani za makazi na kuhesabiwa wakati wa Sensa ya watu na makazi inayotarajiwa kufanyika mwezi Agosti Mwaka huu. Tumeshuhudia elimu ikitolewa kwa njia mbalimbali, nasi wananchi tunalo jukumu la kuipokea elimu hiyo na kuifanyia kazi kwa maslahi mapana ya taifa letu.
Ndugu wageni waalikwa,
Kwa kuwa mkutano huu ni wa kwenu kujadili na kutoa maoni, mimi kazi yangu ni kufungua mkutano huu. Hivyo, sitokuwa na mengi zaidi ya kusema.
Kwa hayo machache, napenda kutamka rasmi kuwa mkutano wa wadau kutoa maoni ya nauli za mabasi umefunguliwa rasmi.
Asanteni kwa kunisikiliza
Amos Makala
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam
13 Aprili, 2022

